DKT. BASHIRU AHIMIZA KAMPENI YA TUTUNZANE KUTATUA MIGOGORO YA WAFUGAJI NA WAKULIMA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewahimiza wafugaji na wakulima kote nchini kuzingatia Kampeni ya Tutunzane inayotekelezwa Wilayani Mvomero inayolenga kuimarisha mahusiano baina yao ili kuepukana na migogoro na uhasama unaotokana na matumizi ya ardhi kati ya Wafugaji na watumiaji wengine wa Ardhi. 

Balozi Dkt. Bashiru ametoa wito huo  leo Machi 06, 2026 wakati  akizungumza na Uongozi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambako amefika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu yaliyomtaka kufika katika Wilaya hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhusiano baina ya wakulima na wafugaji, hivyo amewahimiza kuiga na  kuzingatia kampeni ya tutunzane .

“Mhe. Rais mara nyingi amekuwa akisema hafurahishwi na migogo kati ya wakulima na wafugaji hivyo niwasihi viongozi wenzangu na wakulima na wafugaji tujifunze kupitia kampeni ya tutunzane ya Mvomero ili kuondokana na uhasama huu ambao unaturudisha nyuma.” Alisema Dkt. Bashiru.

Pia, amesema Serikali haitakubali kuona uvunjifu wa sheria ukifanywa  na wakulima na wafugaji huku akisisitiza kuwa mfugaji kutumia maeneo yasiyotengwa kwa ajili ya mifugo na wakulima kutumia maeneo ya mifugo kwa shughuli za kilimo ni ukiukaji wa  sheria na kwamba serikali haitakubaliana na hilo.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Denis Masanja amesema  migogoro ya wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo imekuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi na kupendekeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuanzisha programu maalum za vitalu vyenye miundombinu muhimu kwa ajili ya wafugaji.

Katika ziara hiyo Balozi Dkt. Bashiru ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dkt. Jafar Rajabu Seif pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa  akizingumza na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma baada ya kuwasili leo Machi 06, 2026  kwa Ziara Maalum Wilayani Humo

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Dkt. Jafar Rajabu Seif akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru alipofika kwa Ziara Maalum ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Machi 06, 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Denis Masanja akisoma taarifa ya hali ya sekta za mifugo na uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa alipofika wilayani hapo kwa ziara maalum leo Machi 06, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO