BODI YA MAZIWA YAWAJENGEA UWEZO WATAALAMU WA MIFUGO NA LISHE

 Bodi ya Maziwa nchini imefanya kikao na wadau wa tasnia ya maziwa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo madaktari wa mifugo, maafisa lishe kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe pamoja na wataalamu kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania.

Akizungumza Machi 11,2026 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Msajili wa Bodi hiyo Prof. George Msalya, amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha sekta ya maziwa ili iweze kuchangia zaidi katika kuboresha lishe ya wananchi, kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Amesema kupitia mafunzo hayo, wataalamu hao wanawezeshwa kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na kuwasaidia wafugaji kupata elimu sahihi ya ufugaji bora.

Aidha, Prof. Msalya amesema mafunzo hayo pia yanatoa fursa kwa wataalamu hao kujifunza kuhusu hali ya sasa ya taasisi ya maziwa nchini, mafanikio yaliyopatikana kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili wafugaji na namna bora ya kuzitatua.

Bodi hiyo imefanya kikao hicho na wataalamu walioteuliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 2004, ambapo walipewa jukumu la kuwa wakaguzi wa maziwa katika mamlaka za serikali za mitaa ili kuhakikisha uzalishaji, ukusanyaji na usambazaji wa maziwa unafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa mujibu wa takwimu za sekta hiyo, tasnia ya maziwa imekuwa ikichangia takribani asilimia 2 ya pato la taifa, huku zaidi ya kaya milioni 4.6 nchini zikijihusisha na uzalishaji wa maziwa. 

Sekta hiyo pia imeendelea kuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wafugaji, ambapo mapato yanayotokana na shughuli za maziwa yamefikia takribani shilingi bilioni 4.1 kwa mwaka

Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka, ubora wa maziwa unaboreka na wafugaji wanapata manufaa makubwa zaidi kupitia shughuli zao.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO