TPHPA KUIMARISHA MAHUSIANO NA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) waazimia kuimarisha mahusiano ya kiutendaji kazi katika utumiaji wa teknolojia inayoweza kutambua vinasaba vya virus, bakiteria, fangasi, na vimelea wengine wa magonjwa ya wanyama na mimea (NANOPODS) na matumizi ya ndege nyuki ya ufuatiliaji wa magonjwa.
Akizungumza, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Nchini, Dkt. Benezeth Lutege leo Februari 06, 2026 mara baada ya kutembelea Makao Makuu ya Ofisi ya TPHPA iliyopo Mkoani Arusha, amesema wamejadiliana juu ya matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo na mimea, inayotumika katika mashamba ya parachichi, na kutumika katika ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo.
Aidha, Dkt. Lutege amebainisha wazi kuwa mazungumzo hayo yalikuwa na lengo la kujifunza namna taasisi hiyo ilivyofanikiwa katika kufungua Masoko 408 ya kimataifa ya mazao ya kilimo ndani ya miaka 2.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru ameonesha nia ya kuandaa Hati ya Maelewano (MoU) kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya TPHPA ili kuimarisha mahusiano katika maeneo ya; mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya nanopods na matumizi ya ndege nyuki katika ufuatiliaji wa magonjwa, ufuatiliaji wa pamoja, mikataba ya masoko na eneo la utambuzi na utafiti.


Maoni
Chapisha Maoni