Na. Fausta Njelekela
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya mifugo nchini, kwa lengo la kuboresha mbari za mifugo, kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe, hatua itakayoongeza ubora wa nyama na wingi wa maziwa bora.
Hayo yameelezwa leo Februari 10, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa wakati akizungumza na watendaji wa wizara hiyo katika kikao cha uwasilishaji wa maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).
Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amesema serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa malisho bora kwa njia za kisayansi, ikiwemo kuanzisha na kusimamia mashamba ya malisho ya kisasa pamoja na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kufanya tafiti, uzalishaji wa malisho na mbegu bora za mifugo.
"Tunataka kuwa na maabara ya rufaa ya mifugo kitaifa ambayo ina vifaa, nyenzo na mitambo ya kubaini na kudhibiti magonjwa ya mifugo," amesema Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa
Aidha, Mhe. Balozi Dkt.Kakurwa amewataka wataalamu wa mifugo kuzingatia maadili ya taaluma na kazi zao ili waweze kuwashauri kwa uadilifu na kuwajengea uaminifu wafugaji.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa NAIC, Dkt. Dafay Bura amesema kituo kinafanya kazi ya kuboresha mbari za mifugo kwa kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa mbegu za kisasa kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji, ambapo kwa mwaka 2025/2026 jumla ya mbegu 49,000 zilizalishwa na kusambazwa kwa wafugaji.
Vilevile, Dkt. Bura ameongeza kuwa juhudi hizo zinaambatana na kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya mifugo na wadau wengine wa mifugo nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, katika Kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, Februari 10, 2026 Dodoma.
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Nchini, Ndg. Stephen Michael, akielezea umuhimu wa kupata Madume Bora ya ng'ombe ili kuweza kupata nyama na Maziwa Bora, pamoja na mbinu gani itumike ili kupata Malisho Bora kwa ajili ya Mifugo, katika Kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, Februari 10, 2026 Dodoma, kushoto ni Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dkt. Dafay Bura, akitoa wasilisho linalohusu Masuala ya Uhimilishaji wa ng'ombe, na shughuli zinazofanywa na Kituo cha NAIC, pamoja na Maendeleo yake kiujumla, katika Kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo hicho, kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, Februari 10, 2026 Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa pili kushoto), akisikiliza na kutazama wasilisho la Maendeleo ya Uhimilishaji wa ng'ombe katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) na changamoto zake, katika Kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo hicho, kilichofanyika katika Ukumbi Ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, Februari 10, 2026 Dodoma.
Picha ni watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi (aliyekaa mbele), katika kikao cha uwasilishaji wa Maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za Makao Makuu ya Wizara hiyo, Februari 10, 2026 Dodoma.
Maoni
Chapisha Maoni