RAIS SAMIA: SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI ZISIMAMIWE KISANYANSI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, amewataka Viongozi na Wataalam wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kusimamia sekta hizo kwa misingi ya kisayansi na kisasa ili ziwe chachu ya kuongeza uzalishaji utakaoimarisha usalama wa chakula, kutoa ajira kwa vijana na kuchangia mapato na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mhe. Dkt. Samia ameyasema hayo leo Februari 9, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uapisho wa viongozi wateuli wa nafasi mbalimbali, ambapo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walioapishwa ni Naibu Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya Uvuvi, Prof. Mohamed Ali Sheikh pamoja na Dkt. Fabian Magawa Madele, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya mifugo.
Akizungumza katika hafla hiyo, kwa wateule hao pamoja na wengine Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa sekta za mifugo na uvuvi ni miongoni mwa sekta zenye mavuno ya haraka, hivyo zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mipango ya maendeleo ya taifa.
"Soko la kimataifa linahitaji kwa kiwango kikubwa nyama iliyochinjwa pamoja na mifugo hai, hali inayotoa fursa kubwa kwa Tanzania kuongeza uzalishaji na kuuza bidhaa zake nje ya nchi." alisema Dk.Samia.
Pia amesisitiza kuwa programu ya Jenga kesho iliyo Bora (BBT) katika sekta ya mifugo inapaswa kusimamiwa kwa karibu ili kuwawezesha vijana wengi kufuga kwa tija na kitaalamu, sambamba na kuwaongezea ujuzi wafugaji wengine nchini.
Kwa upande wa uvuvi, Rais Dkt. Samia amesisitiza viongozi kwa kushirikiana na wataalam kusimamia teknolojia za kisasa za uvuvi, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje na kuongeza ushindani wa bidhaa za uvuvi za Tanzania katika soko la dunia.
Aidha, amemtaka Naibu Katibu Mkuu, Prof. Sheikh kutumia uzoefu wake wa sekta ya uvuvi kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na rasilimali za bahari kuu kwa ufanisi na uwazi kwa manufaa ya taifa.

Maoni
Chapisha Maoni