NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI AKAGUA GATI LA KUEGESHEA MELI TAFICO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh amekagua utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa gati la kuegeshea meli (floating jetty), unaotekelezwa na Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), katika Makao Makuu ya Shirika yaliyopo Ras Mkwavi–Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Februari 10, 2026, Prof. Sheikh alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena, ambapo amekagua maendeleo ya mradi huo muhimu unaotarajiwa kuongeza ufanisi wa shughuli za uvuvi na huduma za meli za uvuvi chini ya TAFICO, pamoja na maandalizi ya ujio wa meli ya kwanza ya uvuvi ya Shirika. Akiwa katika eneo la mradi, alimuelekeza mkandarasi wa mradi, kampuni ya Songoro Marine, kuhakikisha kazi zote zilizobakia zinakamilika na mradi huo ukabidhiwe ifikapo tarehe 15 ya mwezi Februari 2026.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Sheikh alisema kuwa kukamilika kwa gati ambao ni miundombinu muhimu katika uendeshaji wa meli ambayo itaingia nchini tarehe 21 Februari, 2026.
“Serikali imewekeza katika ujenzi wa miundombinu hii kuhakikisha mnyororo mzima wa uvuvi unakuwa madhubuti hivyo ni muhimu kwa mkandarasi kukamilisha kazi kwa ubora na kwa wakati kwa kuwa serikali haitaongeza hata siku moja." Alisema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Bi. Perpetua Massaga, akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TAFICO CPA Shaibu Matessa, ameishukuru Serikali kwa ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika.
“Ziara hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha miradi ya kimkakati inayotekelezwa na TAFICO inakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa sekta ya uvuvi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Shirika kupitia menejimenti litahakikisha pia linasimamia vyema utekelezaji wa mradi huu na unakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba." Alisema Bi. Perpetua.
Mradi wa ukarabati wa gati la kushushia meli unatarajiwa kuongeza uwezo wa Shirika la Uvuvi Tanzania katika kuhudumia meli za uvuvi na kuchangia ukuaji wa sekta ya uvuvi na Uchumi wa Buluu nchini.




Maoni
Chapisha Maoni