Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeridhia Upumzishwaji wa shughuli za uvuvi kwa ziwa Tanganyika uendelee kulingana na manufaa yanayopatikana kutokana na takwimu zinavyoeleza.
Akizungumza wakati wa Semina kuhusu upumzishwaji wa shughuli wa Ziwa Tanganyika kwa mwaka 2025 iliyofanyika katika ukumbi uliopo Bungeni jijini Dodoma Machi 28, 2025 Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika amesema wizara iendelee kufanya utafiti katika ukanda wote wa ziwa Tanganyika ili kubaini changamoto na kuzitatua.
Aidha Mhe. Mwanyika ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendele kulinda rasilimali za Taifa kwa manufaa ya Wananchi wake, vilevile amesisitiza kuwa udhibiti wa uvuvi haramu lishughulikiwe kwa nguvu kubwa.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameielekeza kikosi cha kuzuia uvuvi Haramu kuelekea ziwa Tanganyika na kuondoa Nyavu zote zinazotumika kwenye uvuvi Haramu (Gillnet) ili kuendelea kulinda Rasilimali za nchi yetu.
Aidha Mhe. Kijaji ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu manufaa yanayopatikana baada ya zoezi la upumzishwaji wa shughuli za uvuvi ziwa Tanganyika kwa wavuvi pamoja na jamii kwa ujumla ili kuondoa taharuki wakati wa zoezi hilo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amesema Upumzishwaji wa shughuli za uvuvi katika Ziwa ulilenga kurejesha mifumo ya ikolojia kwa kuruhusu idadi ya samaki kuongezeka na hivyo kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wavuvi na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi kwenye pato taifa.
Aidha, Dkt. Mhede ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024, jumla ya tani 85,180.11 zenye thamani ya shilingi bilioni 567.9 za samaki aina ya dagaa, migebuka, kuhe, ngege na wengineo zilivunwa kabla ya kupumzishwa kwa ziwa, baada ya kupumzishwa kwa ziwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi yaliongezeka kwa kiasi cha tani 89,138 zenye thamani ya shilingi bilioni 742.45 zilizovunwa mwaka 2024.
Sambamba na hayo upumzishwaji wa ziwa Tanganyika ulifanyika Mei 15, 2024 hadi Agosti 15, 2024 na kwa mwaka huu unatarajiwa kufanyia Mei 15, 2025 hadi Agosti 15, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni