Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema wizara yake itaendelea
kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inakua kwa kuboresha mialo ya samaki wa maji baridi
na maji chumvi ili kupata samaki bora zaidi na kuongeza masoko ndani na nje ya
nchi.
Prof. Shemdoe amebainisha
hayo leo (05.02.2024) jijini Dodoma kando ya kikao cha katibu mkuu huyo na
wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi
ili kuweka mikakati zaidi ya namna ya kufanya shughuli hiyo kuwa endelevu.
Amesema kutokana na maagizo
aliyotoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
hivi karibuni jijini Mwanza wakati wa kukabidhi boti za uvuvi na vizimba ya
kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na TAMISEMI katika kukuza Sekta
ya Uvuvi, tayari maelekezo hayo yameanza kufanyiwa kazi ili kufikia maono ya Mhe.
Rais.
“Leo hii tumekaa kutekeleza
kimsingi maelekezo ambayo Mhe. Rais ameyatoa na tumepata wasaa kuongea na
wakurugenzi wa halmashauri na kupanga mipango namna bora ya kuimarisha maeneo
ya kupokelea samaki.” Amesema Prof. Shemdoe
Ameongeza kuwa baada ya
kikao hicho kutakuwa na matokeo chanya yakiwemo ya kupatikana kwa bidhaa bora
za samaki ambao watakuwa wanahitajika zaidi kwenye viwanda vya kuchakata minofu
ya samaki hivyo kufanikisha zaidi masoko ya ndani na nje ya nchi.
Awali akifungua kikao hicho
Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Nazael Madalla
amesema Sekta ya Uvuvi imekuwa moja ya chanzo muhimu cha mapato kwa halmashauri
na taifa kwa ujumla pamoja na kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuwa
kichocheo kikubwa cha uwekezaji.
Ameongeza kuwa kufuatia
sekta hiyo kuwa muhimu viwanda vya kuchakata minofu ya samaki vimekuwa
vikihitaji samaki kwa wingi kwa ajili ya kuchakata na kusafirisha minofu ya
samaki katika masoko ya nje ya nchi ambayo yanaliingiza taifa fedha za kigeni,
hivyo ni muhimu kuzilinda rasilimali za uvuvi na kuziongezea thamani.
Nao baadhi ya washiriki wa
kikao hicho wamesema Sekta ya Uvuvi ni muhimu sana katika halmashauri
wanazotoka kwa kuwa sekta hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ajira na
watu wengi wamekuwa wakiishi kwa kutegemea uvuvi.
Wamesema kupitia kikao
hicho watapata fursa ya kufahamu zaidi na namna bora ya kuboresha mialo ya
kupokelea samaki, ikiwemo miundombinu ya kuhifadhia samaki ili kuyaongeza
thamani mazao ya uvuvi.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
inaendelea kukutana na wadau mbalimbali kufuatia maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kutaka Sekta ya Uvuvi kurasimishwa ili wananchi wanaofanya
shughuli zao kupitia sekta hiyo waweze kutambulika rasmi na waweze kunufaika
kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na wakurugenzi wa halmashauri
ya jiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi ili kuweka mikakati zaidi
ya namna ya kufanya shughuli hiyo kuwa endelevu kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Kikao hicho kimefanyika
jijini Dodoma. (05.02.2024)
Kaimu Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Nazael Madalla akifungua kikao cha
wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi
jijini Dodoma ambapo amesema Sekta ya Uvuvi imekuwa moja ya chanzo muhimu cha
mapato kwa halmashauri na taifa kwa ujumla pamoja na kuongeza kipato kwa mtu
mmoja mmoja na kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji. (05.02.2024)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akitoa taarifa ya
hali ya Sekta ya Uvuvi namna wizara inavyofanya jitihada kuhakikisha inatunza
rasilimali za uvuvi, wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma kwa ajili ya
wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi.
(05.02.2024)
Picha ya pamoja ya baadhi
ya wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za
uvuvi na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Nazael
Madalla na baadhi ya wakurugenzi kutoka wizara hiyo baada ya kufungua kikao
kujadili maendeleo ya Sekta ya Uvuvi jijini Dodoma. (05.02.2024)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni