Na. Edward Kondela
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali imedhamiria kuleta
mageuzi makubwa katika Sekta ya Uvuvi, hivyo imeamua kutoa kipaumbele katika
kukuza sekta hiyo kwa kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan amebainisha hayo leo (30/01/2024) jijini Mwanza, wakati wa kukabidhi
boti 160 na vizimba 222 kwa wanufaika kwenye Kanda ya Ziwa Victoria na kuitaka
wizara kubuni mbinu zaidi za kuhakikisha inawezesha wanufaika wengi zaidi
kupitia rasilimali za uvuvi.
Ameongeza kuwa kwa sasa
wizara imekuwa ikifanya mambo mengi makubwa na yenye kuleta tija kwa wananchi
ambapo katika Sekta ya Uvuvi wananchi wengi wamekuwa wakitegemea sekta hiyo kwa
ajili ya kujipatia kipato.
Amewataka pia walionufaika
wa boti za uvuvi na vizimba kuhakikisha wanatumia vyema zana hizo na kuzitunza
pamoja na kuondokana na migogoro yoyote ambayo inaweza kujitokeza kwenye
vikundi vyao kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha mradi huo unaenda maeneo
mengi zaidi hapa nchini.
Aidha, Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024
wizara hiyo ilipatiwa fedha Shilingi Bilioni 60 kila mwaka kwa miaka miwili
mfululizo katika kukuza Sekta ya Uvuvi.
Pia Mhe. Ulega amesema
katika mwaka wa fedha 2024/2025 nia ya wizara ni kusambaza boti za uvuvi
zisizopungua 500 kote nchini ili kuwezesha wanufaika wengi zaidi kwa kuwa Sekta
ya Uvuvi inatoa ajira kwa zaidi ya watu Milioni 4.5.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. Frank Nyabundege amesema Mwaka 2022
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan aliipatia benki hiyo Shilingi Bilioni 210
ambapo nia ya Mhe. Rais ni kuhakikisha benki hiyo inakua na kutatua changamoto
mbalimbali kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Amesema kupitia boti 55
zilizokabidhiwa kwa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya shughuli za uvuvi zitanufaisha
vijana zaidi ya 1,500 na kwamba mikopo ya boti na vizimba inatolewa bila riba
hivyo TADB inatarajia kadri mikopo hiyo itakayovyokuwa inarudishwa
itawanufaisha wengi zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema wizara itahakikisha
inaendeleza maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha
Sekta ya Uvuvi inazidi kutoa ajira zaidi kupitia zana mbalimbali zikiwemo boti
na vizimba ambavyo amevigawa leo kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji kupitia
mkopo usio na riba.
Prof. Shemdoe ameongeza
kuwa kupitia boti na vizimba vijana watapata fursa ya kujipatia ajira pamoja na
kuongezea vipato kupitia ufugaji wa samaki na kwamba kupitia mradi huo jitihada
mbalimbali zitaendelea kufanywa ili kufikia wanufaika wengi zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Mhe. Amos Makala amesema hafla ya kukabidihi boti 55 na vizimba 222 kwa mkoa
huo, utakuza uvuvi endelevu kwa kuwa amekutana na wadau wa uvuvi ambapo tafiti
zinaonesha samaki ndani ya Ziwa Victoria wamepungua kwa asilimia 30 na kuathiri
baadhi ya viwanda vya kuchakata minofu ya samaki, kutokana na kukithiri kwa
baadhi ya matukio ya uvuvi haramu na kwamba mkoa tayari umeweka mikakati
mbalimbali kudhibiti vitendo hivyo.
Mhe. Makala ameongeza kuwa
kitendo cha kuwakabidhi wavuvi boti kitasaidia kukuza uvuvi endelevu na kwamba
elimu imekuwa ikiendelea kutolewa kwa wakazi wa mkoa huo kufuga samaki kwa njia
ya vizimba ili kukuza soko la samaki.
Nao baadhi ya wanufaika wa
boti na vizimba wameshukuru kwa kupatiwa zana hizo pamoja na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki, wameiomba
serikali kuwahakikishia mbegu bora za vifaranga vya samaki pamoja na chakula
ili waweze kufuga kibiashara na kukuza kipato chao na hatimaye kuweza kurejesha
mikopo.
Pia wamesema wamefurahia
kupatiwa boti za kisasa na zenye injini za kupachika ambazo ni imara hivyo
watahakikisha wanatumia vyema boti hizo ili waweze kurejesha mikopo na kuweza
kukopa kwa awamu nyingine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi waliojitokeza
kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki na boti za
kisasa za Uvuvi kanda ya ziwa iliyofanyika leo Januari 30, 2024 uwanja wa
Nyamagana jijini Mwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Wizara muda mfupi kabla ya
kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki na
boti za kisasa za Uvuvi iliyofanyika leo Januari 30, 2024 jijini Mwanza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiwasalimu wananchi na viongozi waliofika
kwenye hafla ya Uzinduzi wa Ugawaji wa Vizimba vya kufugia samaki na boti za
kisasa iliyofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza Januari 30, 2024, Mgeni
Rasmi kwenye Hafla hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan akimkabidhi cheti kiongozi wa kikundi
kilichonufaika na mkopo usio na riba wa
boti ya kisasa za Uvuvi kwenye hafla ya Uzinduzi wa ugawaji wa vizimba
vya kufugia samaki na boti za kisasa kand ya ziwa Victoria iliyofanyika leo
Januari 30, 2024 jijini Mwanza. Katikati anayeshuhudia ni Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni