Nav bar

Ijumaa, 21 Julai 2023

MAUZO YA NYAMA YAONGEZEKA NJE YA NCHI - ULEGA

 Serikali imesema, kiwango cha usafirishaji nyama hapa nchini kimeongezeka hadi kufikia tani 12,243.79 zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 51.894 ziliuzwa nje ya nchi 2022/23 ikilinganishwa na tani 1,774.20 zilizouzwa nje ya nchi 2020/21 .

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega julai 14,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023) ambao unatarajiwa kufanyika Septemba 5-9 mwaka huu jijini Dar es Salaam huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa Ulega ongezeko hilo ni moja ya jitihada zinazofanywa na Rais Samia na wizara yake inaziunga mkono kwa vitendo kupitia Programu ya BBT-LIFE ambapo katika awamu ya kwanza takribani vijana 738 wakiwemo vijana 238 kutoka sekta ya mifugo na vijana 500 kutoka sekta ya uvuvi wamenufaika na mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo ,majongoo Bahari na ufugaji wa Samaki kibiashara.

“Tumejipanga kuongeza uzalishaji Kufuatia jitihada za Rais Samia,tumejipanga kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kuuza ziada ya mazao ya mifugo na uvuvi katika nchi nyingine “amesema Ulega na kuongeza kuwa

“Ujio wa mkutano huo kwa Tanzania ni fursa adhimu ya wadau wetu kukutana na wafanyabiashara mashuhuri na wawekezaji kutoka katika nchi mbalimbali ulimwenguni ,hivyo itasaidia kufungua milango ya uwekezaji na kuongeza mashirikiano ya kibiashara kwa wadau wetu .”

Kwa mujibu wa Ulega mkutano huo pia utatoa fursa za kuona ubunifu na teknolojia mbalimbali ambazo zinazweza kuongeza tia ya uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi.

Aidha amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya maonyesho katika eneo la mkutano kwa lengo la kuonesha shughuli zinazofanyika katika minyororo ya mifumo ya chakula nchini lakini pia kutangaza biashara za wadau ili kupata mitaji na masoko ,hivyo ushiriki wa wadau ni muhimu ili waweze kunufaika na fursa hizo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni