Nav bar

Jumapili, 11 Juni 2023

 SHEKHE WALID, MCHUNGAJI MWAMPOSA MABALOZI UHIFADHI WA BAHARI 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake itawatumia Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shekhe Walid Alhad Omar na Mchungaji wa Kanisa la Arise and Shine na Boniface Mwamposa kuwa mabalozi wa uhifadhi wa Bahari ili wasaidiane nao katika kuelimisha jamii hasa zinazoishi kando ya Bahari juu ya athari ya uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira ya Bahari kwa ujumla.


Waziri Ulega alisema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 8, 2023.


Alifafanua kuwa pamoja na uwepo wa Sheria  kwenye usimamizi na uendelevu wa rasilimali za Bahari, ni muhimu pia kushirikiana na jamii katika kuhakikisha mazingira ya Bahari yanahifadhiwa vizuri kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Alisema kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha jamii wameamua kuwatumia Viongozi hao wa Dini kuwa mabalozi na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuepuka vitendo ambavyo vinapelekea uharibifu wa mazingira ya Bahari.


"Sisi Wizara na Kitengo chetu cha MPRU tupo tayari kushirikiana na viongozi hawa ili waweze kutusaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya athari ya Uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira", alisema


Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde alisema kuwa pamoja na changamoto ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa moja ya kisababishi cha uharibifu wa mazingira ya bahari, yeye pamoja na Waziri Ulega wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia  matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari ili ziendelee kuchangia vyema kwenye uchumi wa buluu.


Kiongozi mwingine wa dini atakayeshiriki kuelimisha jamii ni kutoka Kanisa Katoliki Tanzania, Padri James Ngonyani.


Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika”.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa jamii ya watu wanaoishi jirani na bahari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni