Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema zinahitajika juhudi za pamoja za ndani ya nchi, kikanda na kimataifa katika kuweka mikakati ya kulinda rasilimali za bahari vinginevyo ifikapo mwaka 2050 bahari itakuwa imeelemewa.
Makamu wa Rais alisema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 08 Juni 2023.
Alisema inapaswa kuwepo kwa uwiano sawia kati ya hali ya bahari na kuimarika kwa uchumi kwani Afya ya Bahari na mifumo imara ya kiikolojia ya baharini ni muhimu kwa uchumi wa buluu ambao ni sehemu ya ajenda ya nchi kufikia maendeleo endelevu.
Dkt. Mpango aliongeza kwamba tafiti zinaonesha kufikia 2030 Bahari itakuwa ndio nguzo kuu ya uchumi duniani ambapo takriban watu milioni 40 watakuwa wameajiriwa moja kwa moja na viwanda vinavyotumia rasilimali za bahari.
Aidha, Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi za Utafiti wa Bahari kama Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyoko Zanzibar (IMS) kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika kwa wingi zaidi ili kuongeza uelewa wa sayansi ya bahari pamoja na athari za changamoto zilizojitokeza kwa jamii na ikolojia.
Vilevile Makamu wa Rais amesema upo umuhimu mkubwa wa kuhusisha na kushirikishwa kikamilifu kwa jamii za asili ya pwani katika ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kuwa wao ndio wafaidika au waathirika wa kwanza wa mazingira ya bahari. Pia ameagiza Mamlaka zinazohusika na uvuvi na uhifadhi ziongeze jitihada katika kutoa elimu zaidi kwa wavuvi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali endelevu za bahari na kuondokana na njia zisizofaa za uvuvi.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema Wizara hiyo inatoa umuhimu mkubwa katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za bahari na kudhamiria kuilinda bahari na viumbe wake. Ameongeza kwamba ili kuwa na uvuvi endelevu ni lazima kuwa na maeneo ya uhifadhi baharini ambayo yanalenga katika kulinda, kuhifadhi na kudumisha uvuvi endelevu na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi na pato la taifa.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde alisema kuwa pamoja na changamoto ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa moja ya kisababishi cha uharibifu wa mazingira ya bahari, yeye pamoja na Waziri Ulega wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari ili ziendelee kuchangia vyema kwenye uchumi wa buluu.
Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika” (Planet Ocean: Tides Are Changing)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (kulia) akizindua rasmi Tovuti ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023. Kushoto ni Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini Dkt. Immaculate Sware Semesi na (katikati) ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi, Watumishi, Wadau wa Bahari pamoja na Wananchi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akitoa hotuba fupi wakati akiongea na Viongozi, Watumishi, Wadau wa Bahari pamoja na Wananchi mbalimbali wakati akitoa neno fupi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde akiongea na Viongozi, Watumishi, Wadau wa Bahari pamoja na Wananchi mbalimbali wakati akitoa neno fupi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe akiongea wakati akitoa utambulisho wa Viongozi, Watumishi na Wadau mbalimbali wa Bahari kwenye Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shekhe Walid Alhad Omar (wa pili kutoka kushoto) na Mchungaji wa Kanisa la Arise and Shine na Boniface Mwamposa (wa tatu kutoka kulia) ni miongoni mwa waalikwa walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Bahari yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 8, 2023
Sehemu ya Watendaji wa Wizara wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023
Naibu Katibu Mkuu(Uvuvi), Bi. Agnes Meena (kushoto) akiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023. katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Stephen Lukanga.
Mhifadhi Bahari, Kitengo cha Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu, Mohamed shamte (kulia) akimueleza jambo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kuhusu elimu ya uhifadhi wa Bahari kidigitali katika Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023. Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kitengo cha Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam Juni 8, 2023. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni