Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, uchumi wa buluu ni fursa huku akiwataka wananchi kujipanga na kuweka mazingira muafaka ya uwekezaji ili waweze kunufaika kupitia rasilimali zinazopatikana katika sekta hiyo.
Dkt. Samia alisema hayo katika sherehe za Msimu wa Pili wa Tamasha la Vyakula vya Baharini (Zanzibar Sea Food Festival) lililofanyika katika ufukwe wa Kendwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar Juni 23, 2023.
Wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Rais, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema maana halisi ya uchumi wa buluu ni matumizi endelevu ya rasilimali zilizomo kwenye bahari, maziwa na mito kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa, kutengeneza ajira na kuleta ustawi wa maisha ya watu na vilevile kutunza afya ya maumbile ya bahari.
Alisema kupitia tamasha hilo ni muhimu kujizatiti na kujipanga vyema ili kuweza kuzitumia fursa zilizopo na zinazojitokeza katika sekta ya uchumi wa buluu.
Aliongeza kwa kusema kuwa ili fursa hizo ziweze kuwa endelevu ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na mipango ya matumizi sahihi ya bahari, usimamizi bora wa ikolojia za bahari, kudhibiti uchafuzi wa bahari, kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kusimamia mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini na kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya usimamizi bora wa uchumi wa buluu na rasilimali zake.
Alieleza kuwa ni muhimu kuweka kipaumbele kwenye hifadhi ya mazingira ya bahari kwani bila kufanya hivyo hakutakuwa na upatikanaji endelevu wa samaki na mazao mengine ya bahari.
"Hili sio suala la Kitaifa tu, bali la Kikanda na Kimataifa. kama mnavyofahamu pamoja na kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maeneo yote ya nchi, maeneo ya visiwa yapo hatarini zaidi. Hivyo, hatuna budi kulisimamia vyema suala la uhifadhi wa mazingira," alifafanua
Aidha, alibainisha kuwa mipango ya maendeleo ya Kitaifa imeagiza kutekeleza ajenda ya uchumi wa buluu ya Tanzania, kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa (Vision) 2050 kwa Zanzibar na Dira ya Maendeleo ya 2025 kwa Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni