Nav bar

Jumamosi, 29 Aprili 2023

NDOTO YA RAIS, DKT. SAMIA KUIFUFUA NARCO YAANZA KUTIMIA

Na Mbaraka Kambona,


Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeiwezesha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kiasi cha Shilingi bilioni 4.65 kwa ajili ya kununua vitendea kazi na ng'ombe wazazi ili kuboresha na kuongeza uzalishaji wa kampuni hiyo.


Hayo yamefahamika wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliyoifanya katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Aprili 27, 2023.


Wakati akizindua matreka mapya matano (5) na kupokea ngo'mbe elfu moja (1000) kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa kampuni ya NARCO, Mhe. Ulega alimshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha kampuni hiyo ili iweze kujiendesha kibiashara.


Alisema lengo la Rais, Dkt. Samia ni kuiimarisha NARCO kwa kuboresha miundombinu na vitendea kazi ili waweze  kunenepesha ng'ombe, kuimarisha biashara ya nyama bora ya Kongwa Beef na kuzalisha malisho ya mifugo kwa wingi na kuyauza ndani na nje ya nchi.


"Hivi sasa tumeshafika katika kiwango cha kuuza nje ya nchi nyama Tani Elfu 12, na kuanzia mwaka ujao na kuendelea tutatoka kwenye Tani Elfu 12 na kutafuta Tani Elfu 50 na ikiwezekana mpaka Tani Laki moja", alisema


Aliendelea kusema kuwa katika mkakati wa kuifufua kampuni ya NARCO pia wataanzisha skimu za unenepeshaji wa mifugo ili nyama itakayokuwa inazalishwa kutoka NARCO iwe  na ubora wa kuiuza nje ya nchi.


"Tunakusudia kwamba mchango wa sekta ya mifugo uongezeke kutoka asilimia 7 Hadi kufikia asilimia zaidi ya 10, na hilo linawezekana kwa sababu rasilimali ya kutuwezesha kufikia huko tunayo", alisisitiza 


Aidha, alisema kuwa Serikali ina mipango ya kuanzisha skimu za umwagiliaji wa malisho ili yaweze kuzalisha kwa wingi kwa ajili ya kuyauza ndani na nje ya nchi.


"Kama ambavyo huwa tunasafirisha mahindi kutoka maeneo mbalimbali na kuwapelekea wahitaji tunataka pia tuzalishe malisho kwa wingi na kuyasafirisha kuyapeleka kwa wahitaji waliopo ndani na nje ya nchi", alifafanua

Mkurugenzi Mkuu, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe (kushoto) akimuonesha  Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) sehemu ya vifaa walivyovinunua kwa ajili ya kuzalisha malisho ya mifugo wakati Waziri huyo alipofanya ziara katika  Ranchi ya Kongwa iliyopo Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Aprili 27, 2023. (Kulia) ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega  akimueleza jambo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remidius Emmanuel (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake Wilayani Kongwa, jijini Dodoma Aprili 27, 2023. (Kulia) ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni