Nav bar

Jumamosi, 29 Aprili 2023

MTAMBO WA KUZALISHA KIMIMINIKA NAIC WAZINDULIWA.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia jumla ya fedha Milioni 300 kwa ajili ya kununua mtambo wa Kimiminika (Liquid Nitrogen) kwa ajili ya kuhifadhia mbegu bora za ng'ombe.


Prof.Shemdoe ameyasema hayo Jana  28 April, 2023 wakati  akizindua Mtambo huo wa Kuzalisha Kikiminika  (Liquid Nitrogen) kwa ajili ya kutunzia mbegu bora za ng'ombe wa nyama na maziwa katika kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) Arusha.


"Tunamshukuru sana Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kuridhia jumla ya fedha Milioni 300 ili kujazia katika  fedha  iliyotolewa na Bill & Melinda Gates Foundation Tsh milioni 432  kupitia shirika lisilokuwa la kiserikali la Land O'lakes na kufanya jumla ya Tsh 732 milioni zitumike kununua mtambo huo."Alisema Prof. Shemdoe.


Prof. Shemdoe amesema kuwa kuwepo kwa mtambo huo sasa katika kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) utasaidia kuleta tija hasa  katika kuzalisha ng'ombe bora wa Nyama na Maziwa hapa Tanzania.


"Kwa uwepo wa Mtambo huu hapa NAIC sasa utasaidia kuboresha Mifugo yetu, hivyo kuongeza Uwingi wa nyama bora na maziwa kwani tayari soko la nyama lipo, kwahiyo tukiboresha Mifugo yetu tutapata nyama nyingi na yenye viwango hivyo tutauza nje ya nchi na kuongeza mchango wa Sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa." Alisema Prof. Shemdoe.


Aidha, Shemdoe amesema kuwa zaidi ya asilimia 95 ya ng'ombe waliopo hapa nchini  ni wa asili wenye uzalishaji Mdogo, kwahiyo amesema kuwa  zinahitajika juhudi za Makusudi kuongeza kundi la ng'ombe wanaozalisha nyama na Maziwa kwa wingi ili kutoshereza mahitaji yanayoongezeka ya walaji wa Nyama na Maziwa.


"Azma ya Serikali ya Awamu  ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria  kuboreha Mbari za Mifugo, Serikali imenunua Madume matatu  (3) ya kisasa kutoka Afrika ya kusini pamoja na kuhakikisha kituo hiki  cha NAIC kinakuwa kituo bora cha kuzalisha mbegu za Mifugo Afrika Mashariki na ikiwezeka mbegu hizi ziuzwe hata nje ya nchi."Alisema Prof. Shemdoe.


Awali Kaimu Mkurugenzi wa kituo Cha Taifa Cha uhimilishaji (NAIC) Dkt. Dafay Bura, alimweleza Prof. Shemdoe kuwa kwa sasa kituo kina jumla ya madume bora 34 ambayo yameganyika katika sehemu nne ambazo ni,  Madume ya mbegu ya ng'ombe wa Maziwa,  Nyama na Maziwa (Dual Purpuse), Nyama (Beef) na Cross breed.


Halikadharika, Bill & Melinda Gates pamoja na  Land O'lakes  wamesema kuwa wamefurahishwa kuona mtambo huo wa kuzalisha kimiminika (Liquid Nitrogen) unafanya kazi Vizuri bila shida yoyote, hivyo wanamatumaini makubwa ya kuona wafugaji wanahimilisha mifugo yao ili kujiletea tija mfugaji mmoja mmoja na hatimaye kuchangia katika pato la Taifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe  (kushoto) akishuhudia Kimiminika (Liquid Nitrogen) akizalishwa.Wengine katika picha ni Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akikata Utepe Jana 28 April 2023 kuashiria uzinduzi wa mtambo wa kuzalisha kimiminika (Liquid Nitrogen) katika kituo cha taifa cha Uhimishaji (NAIC) Arusha.Wengine katika picha kutoka kushoto ni Dkt.Afred De Vries, Program  officer BMGF, Dai Harvey, Group Director kutoka Land O'Lakes.

Mtambo wa kuzalisha kimiminika (Liquid Nitrogen) uliozinduliwa jana tarehe 28 April 2023 na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni