Nav bar

Alhamisi, 16 Machi 2023

PROF. SHEMDOE AMSHUKURU MHE.DKT.SAMIA KWA KUTOA TSH BILIONI 266.7

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa jumla ya Tsh. Bilioni 266.7  ikiwa ni gharama ya Ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko Mkoani Lindi.

"Ninamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia Tsh. Bilioni 266.7  ikiwa ni gharama ya Mradi ya Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi hapa Kilwa Masoko Mkoani Lindi." Alisema Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe ameongeza kuwa bandari hiyo ya Uvuvi ikikamilika itakuwa msaada mkubwa sana kwa Watanzania wanaofanya kazi ya uvuvi. Bandari hiyo  itatoa ajira elfu 30 kwa Vijana wa kike na wakiume, itaongeza usafirishaji wa Samaki Nje ya Nchi, itaongeza tija ya Uvuvi Bahari Kuu.

Vilevile, Katibu Mkuu ameainisha faida nyingine kuwa bandari hiyo itapunguza upotevu wa Samaki (Post Harvest), itaondoa changamoto ya uvuvi haramu usioratibiwa na kutolewa taarifa, vilevile itapunguza changamoto ya upungufu wa samaki ndani ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Uvuvi kutoka asilimia 1.71 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 3 mpaka 5 ifikapo 2026.

Pia, Prof. Shemdoe amesema kuwa tayari Mhe. Rais amesharidhia malipo ya awali ya  jumla ya   Tsh. Bilioni 40 na tayari zimeshalipwa kwa Mkandarasi anayejenga bandari hiyo.

Prof. Riziki Shemdoe ameyasema hayo  jana tarehe 13 Machi 2023, alipotembelea eneo la ujenzi wa Bandari  hiyo Kilwa Masoko Mkoani Lindi ambapo mradi huo ni moja ya miradi itakayotembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo tarehe 16 Machi 2023 kwa lengo la kukagua  miradi inayotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mkoani Lindi.

Katika Ziara hiyo Katibu Mkuu amekutana na mkandarasi anayejenga bandari hiyo  kampuni ya  China Harbour Engineering Company Ltd pamoja na Mkandarasi mshauri Elekezi  Dar Al-Handasah Consultants na kuwaelekeza kuwa wafanye kazi kwa bidii ili wamalize ujenzi huo kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mkandarasi anayejenga  bandari hiyo pamoja na Mkandarasi Mshauri mwelekezi wamekubali kuwa watafanya kazi usiku  na mchana ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa.

Awali Prof. Riziki Shemdoe alisema kuwa anamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumhamishia Wizarani ya Mifugo na Uvuvi.

"Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa tena dhamana ya kusimamia Sekta hizi muhimu za Mifugo na Uvuvi, na ninamuahidi Mhe. Rais kuwa nitaendelea kuchapa kazi usiku na mchana ili kuhakikisha Sekta hizi mbili zinasonga mbele na kuchangia mchango mkubwa katika pato la Taifa." Alisema Prof. Shemdoe.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe,(wa nne kutoka kulia) akisikiliza maelezo (Mtoa maelezo hayupo Pichani) nakuangalia ramani ya Bandari ya Uvuvi itakayojengwa Kilwa masoko mkoani Lindi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe wa nne kutoka kulia akijadiliana jambo na timu ya wahandisi wanaotekeleza mradi huo wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi kilwa masoko mkoani Lindi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni