Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema serikali imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili sekta mbalimbali ikiwemo ya uvuvi kufanya kazi kibiashara kwa kuzalisha zaidi bidhaa mbalimbali.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (05.01.2023) jijini Mwanza wakati akishuhudia utiaji saini wa makubaliano baina ya Chama cha Ushirika cha Uvuvi – Bukasiga kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa ambapo Chama cha BUKASIGA kilipata mkopo wa makaushio hayo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB).
Amesema malengo na dhamira ya serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka kuona namna biashara inavyoshamiri hivyo huu ni wakati mzuri wa kuchangamkia fursa ya uwekezaji na kufanya biashara kisasa zaidi na kuongeza bidhaa kwa wingi sokoni zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.
“Uelekeo wa utendaji kazi ndani ya serikali unaweza kuona sisi wasaidizi wa Mhe. Rais tunayo maelekezo wakati wote kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na uwekezaji na hatupaswi kuwa kikwazo kwa namna yoyote.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, ameitaka SUGECO kukisimamia vyema Chama cha BUKASIGA ili mkopo uliyopata chama hicho urejeshwe kwa TADB na chama kuendelea kuaminiwa na kukopeshwa tena kwa kuhakikisha makaushio ya dagaa yanayafanya kazi vizuri na kuliongezea thamani zao la dagaa.
Pia, kufuatia utendaji kazi wa Chama cha BUKASIGA Naibu Waziri Ulega amekiahidi chama hicho kupatiwa na serikali boti ya kisasa na fedha kwa ajili ya utengenezaji vizimba vya ufugaji wa samaki aina ya sato.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Kanali Denis Mwila ameipongeza SUGECO kwa uamuzi wake wa kukubali kukisimamia Chama cha BUKASIGA ili kuhakikisha mtambo wa makaushio ya dagaa unafanya kazi na hatimaye mkopo uliochukuliwa na chama hicho TADB unarejeshwa katika kipindi cha muda mfupi.
Amekishukuru pia Chama cha BUKASIGA namna ambavyo kimekuwa kikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha makaushio ya dagaa yanafanya kazi hivyo ametaka kwa mkataba uliotiwa saini kati ya SUGECO na BUKASIGA makaushio hayo yafanye kazi hadi deni litakapoisha hivyo kutaka uwepo wa ushirikiano zaidi ili wananchi wa Wilaya ya Ukerewe wanufaike kupitia makaushio hayo.
Ameongeza kuwa bila uwepo wa ushirikiano baina ya SUGECO na BUKASIGA ni ngumu kufikia malengo ya mkataba na hatimaye itakuwa vigumu kupatikana kwa matokeo chanya ya uwepo wa makaushio ya dagaa ambayo yanalenga kuliongezea thamani zao la dagaa.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Ushirika wa wavuvi BUKASIGA Bw. Paul Mayunga amesema kuanzishwa kwa kiwanda cha kukaushia dagaa kwa kutumia makaushio ya kutumia mwanga wa jua ambayo bado hayajaanza kazi wameamua kukikabidhi kiwanda kwa SUGECO ikiwa na lengo la kupata uzoefu wa namna ya kutumia mitambo hiyo.
Amesema matarajio ya chama ni kuongeza kipato kwa kutumia uwepo wa zao la dagaa ambalo linavuliwa kwa wingi katika Wilaya ya Ukerewe na dagaa wengi huharibika kutokana na kushindwa kukausha dagaa kwa wingi kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (aliyekaa katikati meza kuu) akishuhudia utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa ambapo Chama cha BUKASIGA kilipata mkopo wa makaushio hayo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB). (05.01.2023)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa pamoja na kuonesha na kuelezea umuhimu wa kukausha dagaa kwa kutumia makaushio ya dagaa ambayo hayaathiri ubora wa dagaa, pia kuelezea namna serikali inavyohakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini. (05.01.2023)
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Kanali Denis Mwila akizungumza wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa ambapo ametaka uwepo wa ushirikiano baina ya BUKASIGA na SUGECO ili mradi huo uwe na tija kwa wananchi hususan wakazi wa Wilaya ya Ukerewe. (05.01.2023)
Afisa Uvuvi Mkuu Bw. Ambakisye Simtowe akifafanua juu ya uwepo wa vyama vya ushirika wa wavuvi nchini pamoja na umuhimu wake wakati wa hafla fupi ya utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa. Katika hafla hiyo Bw. Simtowe alikuwa akimwakilisha Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani. (05.01.2023)
Katibu wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA Bw. Paul Mayunga akielezea juu ya kuanzishwa kwa kiwanda cha kukaushia dagaa kwa kutumia makaushio ya kutumia mwanga wa jua wakati wa hafla fupi ya utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa ambapo Chama cha BUKASIGA kilipata mkopo wa makaushio hayo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB). (05.01.2023)
Muonekano wa baadhi ya wananchi walioshiriki hafla fupi ya utiaji saini makubaliano baina ya Chama cha Ushirika wa Wavuvi – BUKASIGA kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza na Sokoine University Graduates Entrepreneurs Cooperation (SUGECO) kuhusu uendeshaji wa mradi wa makaushio ya dagaa wakisikiliza hoja mbalimbali juu ya mradi huo. (05.01.2023)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni