Nav bar

Jumatano, 18 Januari 2023

BUCHA ZA NYAMA, MINADA YA MIFUGO SASA KUWAHI ZAIDI.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameagiza bucha za nyama za Serikali zilizopo chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufunguliwa saa 12 kamili asubuhi na minada yote ya mifugo iliyopo nchini kufunguliwa kuanzia saa 11 alfajiri ili kuwapa fursa wananchi kupata huduma ya kununua mifugo na nyama mapema.


Mhe. Ulega ameyasema hayo kwenye kikao cha Kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kilichokuwa kikijadili utendaji wa kampuni hiyo na Bodi ya Nyama nchini kilichofanyika leo (17.01.2023) kwenye moja ya kumbi za bunge zilizopo jijini Dodoma.


"Utamaduni wetu tumezoea bucha zinafunguliwa alfajiri kwa sababu nyama tunayonunua inatakiwa kuliwa saa 7 mchana, sasa ukifungua bucha saa 4 asubuhi unataka kumuuzia nani? "Amehoji Mhe. Ulega.


Aidha Mhe. Ulega amebainisha kuwa minada mingi ya mifugo nchini ilikuwa ikianza saa 1 asubuhi ili kuwapa fursa wakaguzi wa mifugo kuweza kuiona mifugo hiyo vizuri ambapo kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya nishati ya umeme kwenye minada mingi iliyopo nchini ukiwemo mnada wa Pugu ameagiza minada hiyo kuanza saa 11 alfajiri.


"Mtu anaenda mnadani saa 10 alfajiri kununua mbuzi wawili au watatu kwa ajili ya nyama choma au supu ya wateja wake anamsubiri Afisa wa serikali ambaye anafika saa 1 asubuhi, hakuwezi kufanyika biashara katika mazingira ya aina hiyo" Amesisitiza Mhe. Ulega.

Akizungumzia kuhusu hatua mbalimbali za kuiboresha Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa changamoto kubwa inayoikabili Taasisi hiyo ni ukosefu wa mtaji ambapo mpaka sasa makadirio ya kiasi kinachohitajika ni takribani Bilioni 440 ambazo zinapaswa kutumika kwenye uhuishaji wa miundombinu mbalimbali.


"Moja ni lazima tuhuishe miundombinu ya ufugaji na uanzishwaji wa skimu za unenepeshaji wa mifugo zenye miundombinu yote inayopaswa kutumika kwenye mnyororo mzima wa kuanzia kwenye unenepeshaji mpaka masoko ya mifugo hiyo" Ameongeza Nzunda.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma mbali na kuipongeza Wizara kwa Taarifa waliyowasilisha, amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kutoa elimu ya uvunaji wa mifugo na kuitunza vizuri ili iweze kuwa na tija kwa mfugaji na Taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda wakiandika dondoo mbalimbali zilizotokana na michango ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa kikao cha pande hizo mbili kilichofanyika leo (17.01.2023) kwenye moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.

Sehemu ya watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wakifuatilia uwasilishwaji wa taarifa ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa kikao cha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kilichofanyika leo (17.01.2023) kwenye moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakimsikiliza mmoja wa wachangiaji wa taarifa ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa kikao cha kamati hiyo na watendaji mbalimbali wa sekta ya Mifugo kilichofanyika leo (17.01.2023) kwenye moja ya kumbi za Bunge jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni