Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemkabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo.
Naibu Waziri Ulega amekabidhi mpango huo leo (19.10.2022)
kwenye Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji
kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma ambapo Taarifa ya Tasnia ya Ngozi
iliwasilishwa.
Akizungumzia kuhusu mpango huo, Naibu Waziri Ulega amesema
kuwa Sekta ya Mifugo imedhamiria kufanya mabadiliko makubwa ambayo yatakwenda
kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji kwa sasa zikiwemo za upatikanaji wa
malisho, maji, majosho pamoja na afya ya mifugo kwa ujumla.
Pia amesema kuwa kwa Tanzania takribani kaya milioni nne hadi
tano zinajishughulisha na shughuli za ufugaji hivyo kwa kutekeleza mpango huo
kutawezesha kaya nyingi kuongeza kipato na kuwezesha ongezeko la mchango wa
Sekta ya Mifugo kwenye Pato la Taifa.
“Sekta ya Mifugo ni Mgodi ambao ukiwekeza leo faida yake
inarudi kwa haraka kwa kuwa Kaya takribani milioni nne hadi tano zinajihusisha
na ufugaji wa kuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe na mifugo mingine hivyo kwa
mpango huu tunatarajia utakwenda kufanikisha utekelezaji wa maelekezo ya Mhe.
Rais Samia wa kuwa na wafugaji badala ya wachungaji wa mifugo,” Alisema
“Lakini kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu
tutahakikisha wadau wanashirikishwa ili waweze kutoa maoni yao yatakayosaidia
kuuboresha zaidi,” aliongeza
Aidha, Wizara hiyo iliwasilisha taarifa ya Taasisi ya Utafiti
wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Taarifa ya Tasnia ya Ngozi kwenye kikao hiyo
ambapo wajumbe wa kamati waliweza kutoa michango yao ambayo Naibu Waziri Ulega
aliwaahidi wajumbe kuwa Wizara itakwenda kuifanyia kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni