Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wajumbe wa bodi ya ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya maziwa nchini ikiwemo kurasimisha sekta hiyo kwa kasi na kuweka vituo ambavyo vitakusanya maziwa Kwa pamoja ili kuondokana na masoko yasiyo rasmi na kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini.
Mheshimiwa Ndaki amezungumza hayo jijini Dodoma
leo Julai 14, 2022 wakati akifanya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya
Maziwa Tanzania ambapo amesema kuwa uzalishaji wa maziwa nchini upo chini
ambapo kwa sasa wastani wa lita bilioni 3.4 ndizo zinazozalishwa huku kiwango
cha unywaji wa maziwa kikiwa ni lita 62 tu kwa mwaka kwa Mtanzania mmoja.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa
nchini Dkt . George Msalya amebainisha mafanikio ya Bodi hiyo mpaka hivi sasa
ikiwa ni pamoja na kukua kwa sekta ya maziwa nchini mpaka kufikia asilimia 2.3,
kuratibu vituo 238 vya kukusanyia maziwa.
"Sekta yetu inakua kwa asilimia 2.3
ikichangia asilimia mbili ya pato la Taifa, uzalishaji wa Maziwa umefikia lita
Bilioni 3.4 kutoka lita Bilioni 1.38 kwa mwaka 2005 wakati ambapo Bodi ilianza
kufanya kazi zake rasmi." amesema Msajili Dkt. Msalya
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri kutoka Bodi
ya Maziwa Prof. Zacharia Samweli Masanyiwa mbali na kumshukuru Mhe. Ndaki
kutokana na imani yake kwake na kuamua kumteua kushika nafasi hiyo, ameahidi
kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mhe. Ndaki kwa kuhakikisha yeye pamoja
na wajumbe wengine wa Bodi kwa wanatumia taaluma zao ili kubadili changamoto
zinazoikabili sekta ya maziwa nchini kuwa fursa.
Kwa upande wake mwakilishi wa Chama cha
Wasindikaji Maziwa Tanzania (TAMPA) Bw. Abdallah Nyalandu amesema anaamini Bodi
hiyo itatatua changamoto walizonazo ikiwemo vifaa vya kusafirishia maziwa.
Kuundwa Kwa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania kunatokana na kutokuwepo Kwa bodi kwa muda wa Miaka minne tangu Bodi hiyo kumaliza muda wake 2019.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni