Edward Kondela
Serikali imesema lengo kubwa la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa wafugaji ni kukuza tija na kuwasaidia kufuga kibiashara ili waweze kunufaika kupitia mifugo yao.
Akizungumza (15.07.2022) wakati akimwakilisha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwenye
maonesho ya mifugo na mnada yanayofanyika katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani
Pwani katika Shamba la mifugo la Mbogo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba
Ndaki amesema shughuli za ufugaji na uvuvi zimekuwa zikiendeshwa kiasili hivyo
kushindwa kukua na kubadili maisha ya wadau wa sekta hizo.
Waziri Ndaki amebainisha kuwa imani mbalimbali
pia zimekuwa zikitawala kwa wafugaji na wavuvi kwenye shughuli zao na
kusababisha kutopokea kwa haraka mabadiliko na kufanya shughuli hizo bila
kufuata utaalamu, ujuzi, weledi na kufahamu hitaji la soko ili kufuga kwa tija
na kibiashara.
“Tumeanza ngazi ya wizara kuzungumza juu ya
tija zaidi na biashara zaidi kubadilisha mtazamo wa wafanyabiashara wetu
wafahamu kufuga ni kazi ya kitaalamu, hivyo natoa wito tuendelee kuelimisha
wafugaji wetu.” Amesema Mhe. Ndaki
Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akizungumza katika maonesho hayo ambayo yamehusisha mifugo bora
na kisasa wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo, amesema fursa ni kubwa sana katika
Sekta ya Mifugo na kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kupatikana kwa wafugaji waliyo
makini katika ufugaji wenye malengo.
Ameongeza kuwa uwepo wa mifugo bora na
inayotambulika ni rahisi kupatikana kwa bidhaa zitokanazo na mifugo ikiwemo
nyama kwa ajili ya soko la ndani na hasa soko la nje ya nchi ili wafanyabiashara
na nchi kwa ujumla kuongeza kipato.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda amebainisha kuwa kupitia mifugo
ni wakati sasa wa kubadilisha wafugaji kutoka kwenye kufuga kiasili na kufuga
kisasa ili waweze kuongeza kipato.
Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itahakikisha
inasimamia malengo yote ya kuwasaidia wafugaji ili Sekta ya Mifugo iwe sehemu
salama kwa wafugaji kuwekeza na kunufaika kimaisha kwa kuongeza kipato kupitia
ufugaji wa kisasa.
Kuhusu ufugaji wa kibiashara, Mwenyekiti wa
Chama cha Wafugaji Kibiashara Tanzania (TCCS) Bw. Naweed Mulla ambao wameandaa
maonesho hayo ya mifugo na mnada ameelezea uanzishwaji wa chama hicho baada ya
kugundua fursa mbalimbali katika Sekta ya Mifugo ambapo wafanyabiashara wa
mifugo walikaa pamoja ili kuchangamkia fursa hizo na kutatua changamoto za
sekta.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni