Tafiti zinazofanywa kwenye sekta ya uvuvi zinalenga kuhakikisha wadau wa sekta hiyo wanaboresha shughuli zao katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.
Hayo yamesemwa leo (25.07.2022) na
mwakilishi wa Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Kayuni ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa sekta hiyo wakati akifungua mafunzo
ya kuandaa vijarida sera yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TAFORI Manispaa ya
Morogoro.
Bw. Kayuni amesema kuwa tafiti
zinazofanyika ni lazima matokeo yake yawafikie walengwa ambao ni wadau wa sekta
ya uvuvi ili kuweza kuwanufaisha na kuboresha shughuli wanazozifanya katika
mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
“Tafiti zinazofanyika ni lazima ziwafikie
walengwa, kuzielewa na kuwasaidia kubalidilisha maisha yao katika shughuli
wanazozifanyi, hapo tafiti hizo zinakuwa na tija katika kuleta maendeleo ya
wadau wa sekta ya uvuvi na taifa kwa ujumla.” alisema Bw. Kayuni
Sekta ya Uvuvi imepanga kuzitumia tafiti
zinazofanywa kwa lengo la kuboresha sera zinazohusu sekta ya uvuvi ili wadau wa
sekta hiyo waweze kunufaika. Bw. Kayuni amesema kuwa tafiti zinazofanywa
zikifanyiwa kazi zinawafanya watafiti kuendelea kufanya tafiti zaidi kwa lengo
la kuboresha sekta ya uvuvi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Huduma za Ugani, Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa mafunzo hayo ni
kwa ajili ya kusaidia kwenye kutunga sera na kufanya maamuzi ambayo yatasaidia
kuipeleka sekta ya uvuvi mbele. Prof. Sheikh amesema Sekta ya Uvuvi imeamua
kufanya mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam ili kuweza
kuzitumia tafiti ambazo zimefanyika ili kuwaletea maendeleo wadau wa sekta
hiyo. Pia amesema kuwa matarajio ya mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa tafiti
mbalimbali zinazofanyika kuhusu sekta ya uvuvi kutobakia kwenye makaratasi badala
yake kwenda kuwafikia wadau na kuleta maendeleo kwenye sekta ya uvuvi.
Meneja Seksheni ya Sayansi za Jamii (COSTECH), Bi. Hildegalda
Mushi amesema kuwa taasisi yao inafanyakazi ya kuwezesha tafiti mbalimbali
ambazo zinalenga kuwezesha maendeleo ya matokeo ya tafiti na kuwezesha
maendeleo ya teknolojia. Tafiti hizi zinalengo la kuhakikisha kuwa wadau wa
uvuvi wanasonga mbele kimaendeleo na kuhakikisha zinawasaidia watunga sera ili
waweze kutunga sera ambazo zinatekelezeka kwa maendeleo ya wadau na taifa kwa
ujumla.
Mafunzo hayo yamewahusisha wataalam
kutoka Sekta ya Uvuvi, Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi (TAFIRI), Wakala ya Mafunzo
ya Uvuvi (FETA), na COSTECH ambapo washiriki wamepata fursa ya kujadili kwa
kina juu ya matokeo ya tafiti zilizofanyika kwa maelengo ya kuipeleka mbele
sekta ya uvuvi.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Prof. Mohammed Sheikh akiwasilisha mada ya utangulizi kwenye mafunzo ya kuandaa vijarida Sera yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TAFORI Manispaa ya Morogoro. Prof. Sheikh amesema kuwa Sekta ya Uvuvi inaendelea kujipanga kuhakikisha matokeo ya tafiti yanakwenda kubadilisha maisha ya wadau wa sekta hiyo. (25.07.2022)
Meneja Seksheni ya Sayansi za Jamii kutoka
COSTECH, Bi. Hildegalda Mushi akizungumza na washiriki wa mafunzo ya kuandaa
vijarida Sera yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TAFORI Manispaa ya Morogoro.
(25.07.2022)
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya kuandaa
viharida sera wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa kwenye mafunzo hayo
yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TAFORI Manispaa ya Morogoro. (25.07.2022)
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Kayuni akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya kuandaa vijarida Sera mara baada ya kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa TAFORI Manispaa ya Morogoro. (25.07.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni