Nav bar

Ijumaa, 29 Julai 2022

SAUDI ARABIA YAKUSUDIA KUWEKEZA KWENYE RANCHI YA RUVU

Nchi ya Saudi Arabia kupitia  kampuni binafsi ya Kilimo ya “Crown” iliyopo nchini humo inakusudia kuwekeza kwenye ranchi ya Ruvu iliyopo mkoani Pwani ikiwa ni hatua ya awali kabla ya kujenga miundombinu ya kusindika mazao ya mifugo nchini.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao baina yake na Mkurugenzi Mtedaji  wa Kampuni hiyo Bw. Mohammad Iftikhar kilichofanyika leo (27.07.2022) kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo jijini Dar-es-salaam.


Mhe. Ndaki amebainisha kuwa ujio wa wawekezaji hao unatokana na uboreshwaji wa shughuli za ufugaji unaoendelea nchini ambao kwa kiasi kikubwa umechochea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya nyama, maziwa na ngozi.


“Nimewaeleza wakutane na kampuni yetu ya ranchi za Taifa (NARCO) na leo mchana watakutana Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo na Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo ili waweze kuzungumza kwa undani kwa sababu fursa za uwekezaji kwenye ranchi zetu za taifa ni nyingi na hata sasa tunafikiria tupate mwekezaji mwingine kwenye ranchi yetu ya Mzeri ambayo tumepanga iwe maalum kwa uwekezaji wa ng’ombe wa maziwa pekee” Amesema Mhe. Ndaki.


Mbali na ranchi za Ruvu na Mzeri, Mhe. Ndaki ameongeza kuwa Wizara yake  ipo mbioni kutafuta mwekezaji kwenye ranchi ya “Mwisa II” iliyopo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambaye atawekeza kwa upande wa viwanda vya nyama, maziwa, chakula cha mifugo na uzalishaji wa malisho ya mifugo.


“Uwekezaji huo unaweza kuwa wa namna mbalimbali kwa sababu sisi tunayo ardhi tunaweza kuwapa kwa makubaliano maalum kisha wao wanaweza kujenga viwanda vya kuchakata nyama, kuzalisha vyakula vya mifugo, walime malisho na ikiwezekana wanaweza kunenepesha mifugo kwenye ranchi zote hizi ili hatimaye wauze wanyama hai au mazao yake” Amebainisha Mhe. Ndaki.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kilimo ya “Crown” kutoka nchini Saudi Arabia Bw. Mohammad Iftikhar amesema kuwa uamuzi wao wa kuwekeza kwenye sekta ya Mifugo nchini unatokana na ongezeko la mahitaji ya nyama nchini Saudi Arabia na mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyopo nchini.


“Kwanza tumevutiwa na suala la NARCO kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100 jambo ambalo linatoa fursa ya kupata wawekezaji stahiki wakati wote na tumepitia andiko linalohusu ranchi zote zilizopo hapa Tanzania na kuona tuanze na Ruvu kisha maeneo mengine yatafuata” Amesema Bw. Iftikhar.


Ujio wa wawekezaji hao ni muendelezo wa matunda yanayotokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo wiki kadhaa zilizopita ambapo aliwaalika wafanyabiashara  mbalimbali kufika nchini na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akimueleza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kilimo ya "Crown" kutoka nchini Saudi Arabia Bw. Mohammad Iftikhar yaliyomo kwenye andiko la Ranchi za Taifa (aliloshika Bw. Iftikhar) wakati wa kikao baina yao kilichofanyika leo (27.07.2022) kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo jijini Dar-es-salaam.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni