Na Mbaraka Kambona, Kilwa
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amewataka Wananchi wa Wilaya ya Kilwa kujiepusha na vitendo vitakavyopelekea kuhujumu ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa na kunufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Telack aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi ya Kilwa baina ya Serikali na Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering (CHEC) iliyofanyika Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Juni 15, 2022.
Alisema kuwa wakati shughuli za ujenzi wa mradi huo utakapoanza wakati wowote kuanzia sasa wanapaswa kuwa walinzi na wajiepushe na vitendo vya udokozi wa vifaa vya ujenzi wa bandari hiyo.
"Niwaombe wananchi wote tuwe walinzi wa shughuli zote zitakazofanyika katika mradi huu, asitokee mtu sasa akaanza kudokoa vifaa vya ujenzi hapa, tutachelewesha mradi huu kukamilika kwa wakati", alisema Telack
Aliongeza kwa kusema kuwa hategemei kuona Mkandarasi analalamika kwamba kuna watu wanafanya vitendo vya wizi katika mradi huo, huku akiwaomba wananchi kutoe ushirikiano kwa wajenzi hao ili mradi huo ukamilike na manufaa yaanze kupatikana mapema kama ilivyokusudiwa.
Aidha, alisema kuwa kwa muda mrefu kazi ya uvuvi imekuwa ikiendelea Wilayani humo lakini manufaa makubwa bado hayajapatikana kutokana na uvuvi huo kuwa na vitendea kazi duni, lakini kwa ujenzi huo wa bandari ya uvuvi anategemea utasaidia kuinua shughuli za uvuvi na soko la samaki kutoka Kilwa litafunguka zaidi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kuwepo kwa bandari hiyo ya uvuvi kutawezesha nchi kunufaika na fursa nyingi za uvuvi katika ukanda wa bahari kuu na hivyo itaongeza uwekezaji katika sekta ya uvuvi na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering (CHEC) ambayo imepewa tenda ya ujenzi wa bandari hiyo, Cheng Yongjian aliishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi hiyo na kusema kuwa wataitekeleza kwa wakati na kuhakikisha ndani ya miezi 24 watakabidhi mradi huo kwa Serikali ukiwa umekamilika.
Baadhi ya wananchi wa Kilwa akiwemo Adam Selemani na Rajab Abdallah ambao wote ni wavuvi walionesha kuwa na matumaini makubwa na mradi huo huku kwa nyakati tofauti wakisema kuwa watahakikisha wanashirikiana na wajenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na ni mategemeo yao kuwa mara mradi huo utakapokamilika utasaidia kuboresha shughuli zao kuliko ilivyo hivi sasa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akimkabidhi mkataba wa ujenzi Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering (CHEC), Cheng Yongjian (kulia) ikiwa ni ishara ya kuikabidhi Kampuni hiyo eneo la ujenzi wa bandari ya Kilwa ili waanze ujenzi muda wowote baada ya makabidhiano hayo.Tukio hilo lilifanyika Juni 15, 2022 Wilayani Kilwa Mkoani Lindi na lilishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni