Watumishi wa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha sekta hizo zinakua
na zinachangia kwa asilimia kubwa katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa
ujumla.
Hayo yalisemwa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki Desemba 17, 2020 katika kikao chake na
watumishi wa wizara pamoja na baadhi ya watumishi wa taasisi na wakala zilizo
chini ya wizara hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo katika mji
wa serikali – Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri Ndaki alisema moja ya
jukumu kubwa walilonalo watumishi wa wizara hiyo, ni kuhakikisha sekta hizo
zinakua ili zichangie kwenye uchumi, ziondoe umaskini wa watanzania na kutoa
ajira.
“Kila mmoja anapofanya kazi
yake ahakikishe anachangia kwenye kutengeneza ajira, kuondoa umasikini wa
wafugaji, wavuvi na watanzania wanaoishi kwa kutegemea sekta hizi na ahakikishe
anafanya kazi ili uchumi wa taifa letu unapande juu ukichangiwa na sekta za
mifugo na uvuvi,” alisema Mhe. Ndaki.
“Wizara inayo mipango mingi
sana ambayo imeandaliwa na baadhi yake tumeshapitishwa lakini kwa sasa
kinachotakiwa ni sote kwa pamoja kuisimamia kuhakikisha inatekelezeka na
inaonekana,” aliongeza Mhe. Ndaki.
Kuhusu sekta ya uvuvi amesema
kipaumbele ni lazima kiwekwe kwenye uchimbaji wa mabwawa pamoja na ufugaji wa
samaki kwenye mabwawa. Yapo mabwawa mbalimbali yanayotengenezwa kwa ajili ya
mifugo, kilimo, umeme na mengine ambapo yangeweza pia kutumika kwa kufugia
samaki bila kuathiri matumizi yaliyolengwa huku akisema umefika wakati sasa
kuanza kuzungumza na wizara nyingine ambazo zina mabwawa ili ufugaji huo uweze
kufanyika.
Mhe. Ndaki alipongeza
jitihada na kazi nzuri inayofanyika ya
kuzuia uvuvi haramu kwani uvuvi huo umekuwa ukileta madhara makubwa hasa pale
ambapo wavuvi walikuwa wakitumia mabomu huku akiagiza udhibiti wa uvuvi haramu
ni lazima uendelee lakini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili
kutoleta migogoro wakati wa usimamizi wa rasilimali za uvuvi.
Kwa upande wa sekta ya mifugo
alisema nguvu kubwa inatakiwa kuwekwa kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia
mazao ya mifugo kwani utasaidia kubadilisha aina ya ufugaji kwa wafugaji kwa
kuwa watakuwa na uhakika wa wapi soko la ng’ombe bora lilipo na faida zake
jambo ambalo litafanya kutotumika nguvu kubwa kuwahamasisha wafugaji kutoka
kwenye ufugaji wa ng’ombe wa kienyeji na kuingia kwenye ng’ombe bora.
Aidha, Waziri Ndaki amewataka
watendaji wa sekta ya mifugo kuangalia namna ya kuwa na mbegu bora ya malisho
ya mifugo ambayo wafugaji watakuwa na uwezo wa kuimudu na kwa kufanya hivyo
watakuwa wamewasaidia wafugaji kuwa na malisho ya uhakiki na hivyo kupunguza au
kuondoa kabisa tatizo la wafugaji kuhamahama linalosababisha migogoro na
watumiaji wengine wa ardhi.
Naye Naibu Waziri wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi
wa wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kwani ndio njia pekee itakayoisadia
wizara hiyo kutimiza malengo yaliyowekwa katika kuhakikisha wafugaji, wavuvi na
taifa kwa ujumla linapata maendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa wizara ina watumishi
wachapakazi na wenye uvumilivi hivyo ni matarajio yake kuwa ushirikiano uliopo
utaendelezwa kwa viongozi wapya huku akisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi
yaliyofanyika sio adhabu wala zawadi kwa mtu yoyote ni majukumu ndivyo
inavyobidi yaende.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah asema kikao hicho cha
watumishi kimesaidia sana kwani watumishi sasa wamesikia kutoka kwa viongozi
wao ni njia ipi itakayotumika katika kufanikisha malengo ya wizara yaliyowekwa.
Pia amewahakikishia Mawaziri kuwa watumishi wa wizara watatumia weledi wao
katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Picha ya pamoja ya baadhi ya
wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa na viongozi wakuu, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul, Katibu
Mkuu Sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel na Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi,
Dkt. Rashid Tamatamah baada ya kikao na wafanyakazi wa wizara hiyo wakiwemo
wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara, kilichofanyika kwenye
viwanja vya ofisi za wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma.
(17.12 2020)
Baadhi ya wafanyakazi wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwemo wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya
wizara, wakiwasikiliza viongozi wakuu wa wizara wakati wa kikao cha kwanza na
wafanyakazi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri,
Mhe. Pauline Gekul, kikao kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara
hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma. (17.12 2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo wakiwemo
wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara (hawapo pichani), wakati wa kikao na
wafanyakazi kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara hiyo katika mji
wa serikali Mtumba jijini Dodoma na kusisitiza ushirikiano na kufanya kazi kwa
kasi ili kufikia malengo ya serikali kupitia sekta za mifugo na uvuvi. (17.12
2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akimuongoza Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, wakifuatiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe.
Pauline Gekul na Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah
kwenye viwanja vya wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma kwa
ajili ya kikao na wafanyakazi wa wizara. (17.12.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wafanyakazi wa
wizara hiyo wakiwemo wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara (hawapo
pichani), wakati wa kikao kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara
hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma na kuwasifu wafanyakazi wa
wizara hiyo kwa utendaji wao wa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa
bidii. (17.12 2020)
Wafanyakazi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi wanaofanya kazi katika makao makuu ya wizara hiyo jijini
Dodoma, pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara wakiwa
wamesimama wakati viongozi wakuu wa wizara (hawapo pichani) wakiongozwa na
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakiwasili kwenye viwanja vya
ofisi za wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba kwa ajili ya kikao na
wafanyakazi. (17.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo wakiwemo wakuu wa
taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara (hawapo pichani), wakati wa kikao chake cha kwanza na
wafanyakazi kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara hiyo katika mji
wa serikali Mtumba jijini Dodoma na kusisitiza uwajibikaji pamoja na
kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinaleta tija katika taifa na ajira kwa
wananchi. (17.12 2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wafanyakazi wa wizara
hiyo wakiwemo wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara, wakati wa
kikao kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara hiyo katika mji wa
serikali Mtumba jijini Dodoma na kuelezea kufurahishwa na ushirikiano uliopo wa
viongozi wenzake wa wizara na wafanyakazi. (17.12 2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni