Taasisi zinazohusika na
utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini
Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) wamekutana kujadili na kufanya
tathimini ya utekelezaji wa mradi huo wa miaka sita (6) ili kupima mafanikio na
mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kufanya maamuzi ya kuendelea na awamu ya pili
ya utekelezaji wake.
Akitoa taarifa fupi ya
utekelezaji wa Mradi huo kwa wadau waliohudhuria kikao hicho kwa njia ya
mawasiliano ya kimtandao (Web conference) kutokea jijini Dodoma Disemba 16,
2020, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema
kuwa kikao hicho cha tathimini ni moja ya taratatibu walizoziweka kuwa kila
baada ya miezi sita timu ya wataalamu kutoka taasisi za utekelezaji pamoja na
wafadhili wa mradi huo Benki ya Dunia wanakaa pamoja kutathimini maendeleo ya
mradi huo ili kusaidia kusukuma utekelezaji pale ambapo pataonekana kuna
mkwamo.
“Kwa ujumla niseme tangu
mradi huu uanze hatujawahi kupata taarifa isiyoridhisha kutoka kwa wafadhili wa
mradi, wamefurahishwa na utekelezaji unavyoendelea kwenye maeneo yote ikiwemo matumizi ya pesa,
na ujenzi wa majengo mbalimbali na inatupa faraja kuona kwamba tunatekeleza
mradi huu kama tulivyokubaliana,” alisema Dkt. Tamatamah
Dkt. Tamatamah alisema kuwa
wameshawasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha kuongeza muda wa utekelezaji wa Mradi
huo kwa mwaka mmoja zaidi badala ya kuisha mwaka 2021 uendelee mpaka 2022 ili
kufidia mapungufu yaliyojitokeza kufuatia
athari za mlipuko wa ugonjwa wa
Korona ulioikumba Dunia mwanzoni mwa mwaka huu huku akisema Benki ya Dunia
imeridhia ongezeko hilo la muda ili mradi huo uweze kutimiza adhma yake.
Aliendelea kusema kuwa
kufuatia vikwazo vya kusafiri vilivyoweka katika baadhi ya maeneo ya nchi
duniani kutokana na maradhi ya Korona wameamua kufanya vikao kupitia
mawasiliano ya kimtandao na vikao hivyo vilianza tangu Disemba 14, 2020 ambapo
wadau wamekuwa wakikutana kujadili maendeleo ya mradi huo na Disemba 18, 2020
ndio ilikuwa hitimisho kwa wadau wote kupitia taarifa ya utekelezaji na
kukubaliana mambo ya msingi ya kufanya kabla kuendelea na utekelezaji kwa muda
ulioongezwa.
Aidha, Dkt. Tamatamah
aliongeza kwa kusema kuwa Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia Tanzania
kufanikisha mpango wake wa kutekeleza agenda yake ya uchumi wa Bluu huku
akisema kuwa Wizara ipo tayari kuendelea kushirikiana na Benki hiyo katika
kulinda rasilimali za uvuvi na kuleta maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa ujumla.
Taasisi zinazotekeleza
mradi huo ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania Bara, Wizara Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu zote kutoka
Zanzibar.
Mradi huo wa SWIOFish tangu
uanze kazi mwaka 2015 umekuwa ukitekeleza shughuli mbalimbali zinazohamasisha
ulinzi wa rasilimali za bahari ikiwemo usafi wa fukwe za bahari, ujenzi wa
majengo ya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) pamoja na ununuzi wa
vifaa mbalimbali kama vile Boti ambazo zimesaidia kukomesha uvuvi haramu katika
maeneo mbalimbali na kusaidia kutoa
huduma kwa watalii nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa maelezo kuhusu kikao kifupi cha tathmini ya Maendeleo ya Mradi wa SWIOFish toka umeanza hadi sasa, na ambapo akielezea jinsi Benki ya Dunia ilivyofurahishwa kwa namna mradi huo ulivyoendeshwa. Kikao hicho kimefanyika Disemba 18, 2020 kwenye ukumbi wa NBC, jijini Dodoma.
Afisa
Uvuvi Mwandamizi, Bi. Upendo Hamidu akifafanua jambo wakati wa kikao cha
kufanya tathmini ya Maendeleo ya Mradi wa SWIOFish Kati ya Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Taasisi zinazotekeleza Mradi kwa Tanzania bara , Zanzibar na Mamlaka ya
Bahari kuu kilichofanyika jijini Dodoma Disemba 18, 2020.
Sehemu
ya Wajumbe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Taasisi zinazotekeleza Mradi wa
SWIOFish Tanzania Bara na Visiwani pamoja na Mamlaka ya Bahari Kuu wakiwa
katika kikao cha majadiliano na Viongozi wa Benki ya Dunia kwa njia ya Mtandao
kuhusu kufanya tathimini ya Maendeleo ya Mradi wa SWIOFish kilichofanyika
jijini Dodoma Disemba 18, 2020. Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni