Wataalamu wa Mifugo wanaosimamia machinjio nchini wametakiwa kuhakikisha wachunaji wa Ngozi za Wanyama wawe ni wale waliopata mafunzo na wamepewa Leseni ya uchunaji ili ngozi inayochunwa iwe na ubora utakaofaa kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Stanford
Ndibalema alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika Kikao kazi cha
Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika
kutekeleza mikakati ya sekta ya mifugo kuendana na Ilani ya Chama Tawala
kinachofanyika Mkoani Singida Disemba 16-17, 2020.
Dkt. Ndibalema alisema kuwa
ubora wa ngozi unaanzia shambani, hivyo wajibu wa kwanza ni wa Mfugaji mwenyewe
kuhakikisha wanyama wanapatiwa matunzo mazuri ikiwemo chakula, chanjo na
kuogeshwa kwa wakati ili kuwakinga na magonjwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndibalema,
Serikali imeshatunga Sheria na kanuni ambayo inawataka wachunaji wa ngozi wawe
ni watu wanaotambulika na wamepewa leseni ya uchunaji ili kazi ya uchunaji iwe
rasmi na ifanywe kwa weledi ili kupata ngozi bora na yenye thamani sokoni.
“Sehemu kubwa ya machinjio
nchini zinamilikiwa na Serikali za Mitaa, hivyo niwaombe viongozi wa serikali
za mitaa na hasa Wataalamu wanaosimamia machinjio kuhakikisha wale wanaojishughulisha
na uchunaji wa ngozi wawe wamepata mafunzo na wamepewa leseni ya uchunaji,
tunaamini hayo yote yakizingatiwa ngozi hazitaharibiwa wakati wa uchunaji na
hivyo tutapata ngozi bora itakayokuwa na thamani sokoni,” alisema Dkt.
Ndibalema
Naye, Afisa Mifugo kutoka
Mara, Denis Ishengoma alisema kuwa ili afya ya Wanyama iwe bora na kutoa mazao
mazuri ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji na wachunaji wa ngozi na
Halmashauri itenge bajeti ya kuboresha afya za mifugo.
“Ngozi zinazalishwa lakini
nyingi hazina ubora na thamani ya kuuzika sokoni, hivyo naiomba Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inasimamia eneo hili vyema ili mazao ya ngozi yawe
na ubora na yatafutiwe masoko ndani na nje ya nchi,” alisema Ishengoma
Kwa upande wake, Daktari wa
Mifugo kutoka Mkoani Morogoro, Gasper Msimbe alisema kuwa sheria ya utambuzi wa
mifugo na ufuatiliaji Namba. 12 ya Mwaka 2010 imeelekeza eneo la kuweka alama
kwa mnyama hivyo Halmashauri zielimishe wafugaji wasiweke alama katika maeneo
ambayo yataharibu thamani ya ngozi.
“Ili kuhakikisha hawa
wafugaji wanatii, tunaiomba Wizara iweke kanuni kwamba mifugo iliyowekwa alama
inayopunguza thamani ya ngozi isipelekwe kuuzwa mnadani, hii itakuwa njia moja
wapo ya kudhibiti uwekaji wa alama katika maeneo ambayo yanaharibu thamani ya
ngozi,” alisema Dkt. Msimbe
Aidha, Afisa Mfawidhi wa
Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo, Kanda ya Kusini Magharibi, Rukwa,
Dkt. Kaini Kamwela alisema kuwa wakati umefika sasa kama nchi kuwa na mkakati
mzuri wa kibiashara wa zao la ngozi utakaoweza kuainisha mambo mbalimbali
yatakayowezesha ngozi kuuzwa nje ya nchi.
Awali akifungua Kikao kazi
hicho cha siku mbili, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Deogratius Yinze
aliwataka wataalamu hao wa mifugo kuhakikisha wanaendelea kutoa utaalamu wao
ili kuendeleza sekta ya mifugo iweze kuleta tija katika uzalishaji na kuchangia
vyema katika uchumi na pato la taifa.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi,
Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah
akitoa maelezo mafupi kuhusu Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na
Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi cha kujadili utekelezaji wa Mikakati ya
Sekta ya Mifugo kuendana na Ilani ya Chama Tawala kinachofanyika Mkoani Singida
Disemba 16 -17, 2020. Kulia ni Kaimu
Katibu Tawala, Mkoa wa Singida, Deogratius Yinza. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi
wa Sera na Mipango, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbaraka Stambuli.
Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa
Singida, Deogratius Yinza akiongea na washiriki wa Kikao kazi cha Washauri wa
Mifugo wa Mikoa na Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati akifungua
kikao hicho kinachofanyika Mkoani Singida kuanzia Disemba 16 - 17, 2020. Lengo
la kikao kazi hicho ni kujadili mikakati ya utekelezaji wa sekta ya Mifugo
itakayoenda sambamba na Ilani ya Chama Tawala. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara
ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(ORTAMISEMI), Mhandisi Enock Nyanda. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi,
Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri
Gillah.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya
Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(ORTAMISEMI), Mhandisi Enock Nyanda akieleza jambo wakati akiongoza kikao kazi
cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi cha
kujadili utekelezaji wa mikakati ya Sekta ya Mifugo kuendana na Ilani ya Chama
Tawala kinachofanyika Mkoani Singida Disemba 16- 17, 2020. Kulia ni Afisa
Utafiti wa Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Grace Masolwa.
Kaimu Katibu Tawala, Mkoa wa
Singida, Deogratius Yinza (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na
Washiriki wa Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na Wataalamu wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi cha kujadili utekelezaji wa Mikakati ya Sekta ya Mifugo
kuendana na Ilani ya Chama Tawala kinachofanyika Mkoani Singida Disemba 16 -
17, 2020. Kutoka kulia waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Stanford Ndibalema na wapili kutoka kulia ni Kaimu
Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI), Mhandisi Enock Nyanda. Kutoka kushoto ni Afisa
Mifugo Mkuu, Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza, Candidah Kyamani na wapili ni
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah.
Afisa Mifugo Mkuu, Idara ya
Uzalishaji wa Mifugo na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mariam Muchakila
akiwasilisha mada katika Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo wa Mikoa na
Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi cha kujadili utekelezaji wa Mikakati ya
Sekta ya Mifugo kuendana na Ilani ya Chama Tawala kinachofanyika Mkoani Singida
Disemba 16- 17, 2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni