Mkufunzi Mkuu wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gilla amesema ni vema kufanya kilimo cha malisho ya mifugo kwa mzunguko katika eneo moja kwa muda usiozidi miaka mitano ili kuzalisha kwa wingi na kupunguza kiwango cha magugu.
Dkt. Gilla alisema hayo
wakati wa ziara ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye shamba la
malisho la Langwila lililopo mkoani Mbeya walipotembelea kujionea shughuli
zinazoendelea shambani hapo.
"Tusibuni namna ya
kuotesha malisho bali twende kwa utaratibu unaotakiwa na hii itasaidia kupata
muda wa kurutubisha ardhi na kupata malisho yaliyo bora," Alisema Dkt.
Gilla
Hata hivyo Dkt. Gilla amesema
ili kuweza kuwa na mbegu bora ni vyema kuvuna kwa wakati, kuchakata na
kuhifadhiwa vizuri ili kuepuka kuoza kwa mbegu na kuwa na utaratibu wa
kuhakikisha ubora wa mbegu za malisho.
Aidha, alishauri kupitia Idara
ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo isaidie
kutengeneza duka la malisho pembezoni mwa Barabara kuu ili kujitangaza na
kusaidia watu kupata huduma kwa ukaribu zaidi na kuweza kuongeza pato la shamba
na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Sera na Mipango, Bw. Amos Zephania alisema ili uzalishaji uwe bora na wa tija
ni vyema wafugaji wakapewa elimu ya upandaji na ulimaji wa malisho kwa vitendo
ili kuongeza ufanisi zaidi.
"Tunahitaji kutumia
miundombinu yetu vizuri ili kuweza kujipatia fedha za kuendesha shamba letu kwa
kukodisha matrekta kwa wakulima," Alisema Bw. Zephania
Aliongeza kuwa mikataba ya
kukodisha matrekta kwa wakulima iandaliwe kwa kuonyesha idadi za ekari
zilizokodishwa na kwa kiasi kilichopendekezwa.
"Mashamba yasikodishwe
kwa kufikiria tuu bali ni vyema kuwasiliana, kupata mwongozo na ni vyema pia
Katibu Mkuu Mifugo alifahamu hili ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima,"
Alisisitiza Bw. Zephania
Naye Meneja wa shamba la
Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander aliwashukuru watumishi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa kufanya ziara shambani kwao na kupokea yale yote waliyofundishwa
na kuelekezwa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa wakati.
Kaimu Mkurugenzi wa
Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Steven Michael
akichangia hoja wakati wa ziara ya kutembelea shamba la malisho la Langwila mara
baada ya kutembelea stoo iliyojazwa mbegu za malisho na kushauri kuangalia
namna bora zaidi ya kuhifadhi mbegu hizo. (16.09/2020)
Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Mayage akikagua faili la kumbukumbu
ya manunuzi ya vifaa kwenye shamba la malisho ya mifugo Lagwila, mkoani Mbeya
walipotembelea shambani hapo. (16.09.2020)
Afisa Utumishi Mwandamizi
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Andrew Ponda (katikati) akiwakumbusha
watumishi wa shamba la Langwila juu ya ujazaji wa fomu za opras na umuhimu wake
walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Bw. Ephron Sanga (kushoto) akipata maelezo ya namna ya
kukusanya malisho, kuyafunga kwenye marobota na kuhifadhi kwa ajili ya kuuza.
(16.09.2020)
Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha
Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt. Edwin Chang'a (wa nne kutoka kulia) akiwatembeza watumishi
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho wakati wa ziara
yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)
Afisa Mifugo Mkuu kutoka
Wizara ya Mifigo na Uvuvi, Bw. Israel Kilonzo akifungua kikao cha kujadili
namna wanaweza kusaidia shamba la malisho Langwila kufanya vizuri zaidi ikiwa
ni pamoja na ushirikiano baina yao, walipotembelea shamba hilo lililopo mkoani
Mbeya na kuona shughuli zinazoendelea. (16.09/2020)
Watumishi wa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi wakiangalia ndama katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ndama mara
baada ya kuzaliwa ambapo hupewa huduma na uangalizi wa karibu. (16.09.2020)
Meneja wa shamba la malisho
ya mifugo Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander akieleza namna mashine ya
kukatia nyasi inavyofanya kazi kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)
Mtunza Kumbukumbu Msaidizi
kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi, Bi. Nsia Kileo akichangia mada kwenye kikao
kifupi kilichofanyika kwenye shamba la malisho Langwila mkoani Mbeya. (16.09.2020)
Watumishi kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa shamba la mbegu
za malisho ya mifugo Lagwila walipotembelea kujifunza na kujionea mazingira na
shughuli zinazofanywa katika shamba hilo. (16.09.2020)
Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha
Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt. Edwin
Peter Chang'a akiongea na watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo
pichani) walipotembelea kituo hicho wakati wa ziara yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)
Watumishi wa Wizara ya mifugo
na Uvuvi wakielekea kuangalia jengo kwa ajili ya Kiwanda kidogo cha uchakataji
wa Maziwa ambalo bado lipo kwenye ujenzi kwenye kituo cha Utafiti wa Mifugo
Uyole (TALIRI) mkoani Mbeya. (16.09/2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni