Nav bar

Jumatano, 16 Septemba 2020

WATAALAM WA MIFUGO WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.

 Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga amewasihi watumishi wa umma kuwa wazalendo kwa kutimiza wajibu wao na kuwatia moyo kwamba wapo hapo kwa makusudi ya Mwenyezi Mungu.

 

Prof. Nonga amesema hayo katika shamba la kuzalisha mitamba Saohill Mkoani Iringa wakati wa majadiliano ya namna watakavyoboresha na kufanya shamba hilo kuzalisha zaidi na kupata mafanikio makubwa.

 

"Kutotimiza yale mnayopaswa kufanya ni dhambi kama dhambi zingine na tukiendelea kuwaza hasi hatutakuwa wazalendo na wala hatutaendelea,” Alisema Prof. Nonga.

 

Prof. Nonga amesisitiza kutengenezwa kwa programu nzuri itakayosaidia kujua magonjwa ya mifugo ili kusaidia kutoeneza magonjwa kwa mifugo mingine na kuwa na utaratibu wa kuchanja mifugo kila mara.

 

"Tuwe na mikakati ya kutambua magonjwa ili kusaidia katika udhibiti wa magonjwa na vifo pamoja na uongozi mzuri ili kusaidia shamba kuendelea," alisisitiza Prof. Ezron Nonga.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Stephen Michael amewataka watumishi hao kujitathmini na kuona ni wapi wametoka na wanapoelekea katika uzalishaji, uboreshaji na uendelezaji wa shamba la Saohill na sio kufanya mambo kwa makadirio ambayo husababisha kuendelea kushuka kwa uzalishaji katika shamba hilo.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Fraksed Mushi amewakumbusha watumishi wa shamba la mitamba Saohill kufuata sheria, na kusisitiza kuwa likizo ni muhimu na lazima kwa kila mtumishi kwani ni haki kisheria.

 

"Likizo za uzazi kwa mwanamke ni siku 84 na kwa upande wa mwanaume ni siku tano (5)," alimalizia Bw. Mushi.

 

Aidha, watumishi katika shamba la Saohill wamewashukuru watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwaelimisha na kuwapa uelewa kwenye mambo ambayo walikuwa hawayajui na kukumbushwa baadhi ya maadili wanayopaswa kuyaishi  kwenye utumishi wa umma.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga awaasa wafanyakazi kuwa wazalendo na kufanya yale wanayopaswa kufanya kwenye ofisi za shamba la Saohill walipoenda kutembelea na kujifunza mambo mbalimbali kwenye shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Steven Michael akifungua mjadala wa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wafanyakazi wengine wa shamba la Saohill kwenye ofisi za shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiangalia baadhi ya mashine zinazotumika kwenye shamba ya Saohill kwa ajili ya kukatia, kukusanya na kufunga malisho kwenye karakana ya shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya mifugo na Uvuvi wakipima uzito wa marobota ya malisho ya mifugo kwa kuyabeba walipotembelea shamba la Mifugo la Saohill Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Baadhi ya malisho ya Mifugo   waliyovunwa na kufungwa kwenye marobota 1,200 katika shamba la Saohill tayari kwa kubebwa na kwenda kuhifadhiwa. (15.09.2020)

Mabanda kumi na mbili ya madume yanayofahamika kama NAIC 2 yenye uwezo wa kuweka madume 24, yapo katika shamba la Saohill Mufindi Mkoani Iringa. Lengo lilikuwa ni kuhifadhi madume ila hadi sasa hakuna mfugo wowote unaoishi huko. (15.09.2020)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni