WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina amezindua kwa pamoja vituo viwili vya Uchunguzi wa Magonjwa ya
Mifugo (ZVC) na Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Kanda ya Magharibi-
Sumbawanga na kutangaza msimamo wa Serikali ya awamu ya tano wa kupambana na
magonjwa ya mifugo ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao yake nchini.
Hivyo Serikali
inawahakikishia wananchi uhakika wa upatikanaji wa chanjo kwa bei nafuu kutokana
na uwekezaji mkubwa unaofanyika ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Chanjo (TVI)
kuzalisha chanjo za kimkakati 11 ifikapo Juni mwakani na kwamba Serikali iko
mbioni kutangaza bei elekezi ya Chanjo ili kuwadhibiti watu wachache waliokuwa
wanawaibia wananchi.
Aliongeza kuwa hivi sasa
kuna ujenzi mkubwa wa Kiwanda kipya cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience
Africa Limited (HBAL) ambacho kitazalisha chanjo 27 ifikapo Juni na uwekezaji
wake una thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 50 na kuwezesha upatikanaji wa
chanjo zote kwa wafugaji wa ndani ya nchi, Afrika na Dunia.
Akizungumza mara baada ya
kuzindua vituo hivyo vitakachohudumia mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi vyenye
makao yake mjini Sumbawanga, Waziri Mpina amesema kamwe Serikali haiwezi
kukubali mifugo iendelee kufa kwa magonjwa na kwamba sasa magonjwa hayo hayana
nafasi tena nchini.
Hivyo Serikali imeamua
kuandaa Kanuni mpya za usimamizi wa uogeshaji na uchanjaji mifugo ili kudhibiti
utoaji wa chanjo kwa wananchi na kwamba itaendelea kuchukua hatua kali za
kisheria kwa wote wataokwenda kinyume na kanuni hizo.
Hivyo ameziagiza
halmashauri zote nchini kuhakikisha zinashirikiana kwa karibu na vituo vya
uchunguzi wa magonjwa na wakala wa maabara ya magonjwa ya mifugo vilivyoko
katika kanda zao ili kutoa huduma bora kwa wafugaji na kuongeza uzalishaji wa
mifugo na mazao yake.
Waziri Mpina pia amemuagiza
Katibu Mkuu Mifugo na Katibu Mkuu Tamisemi kufanya mgawanyo mpya wa maafisa
mifugo ili kuweza kupelekwa kwenye maeneo ambayo hayana kabisa maafisa mifugo ukiwemo
Mkoa wa Katavi ambao hauna kabisa Madaktari wa Mifugo.
Pia ameagiza ZVC na TVLA
Kanda ya Magharibi Sumbawanga kuwa wasimamizi na walezi wazuri wa wafugaji na
mifugo na kuhakikisha kuwa chanjo, uogeshaji na haki za mifugo zinasimamiwa
kikamilifu.
Waziri Mpina pia ameiagiza
Kanda kusimamia kikamilifu uingizaji wa chanjo, madawa, viuatilifu, chakula na
mazao ya mifugo yanayoingizwa nchini bila vibali, bila kulipiwa ushuru, bila
kukaguliwa na yaliyokwisha muda wa matumizi na feki.
Kufuatia mageuzi ya utoaji
huduma za mifugo nchini, Waziri Mpina amemwagiza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo
kufanya ukaguzi wa maafisa wa kanda zote ili kupanga safu mpya itakayokuwa
tayari kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Waziri Mpina ameonya kuwa
siku nyingine ikitokea hatua zikachelewa kuchukuliwa kwa maafisa wanaohujumu
mifugo basi Mkurugenzi wa huduma za mifugo ataondolewa kwenye wadhifa wake.
Waziri Mpina alisema
wafugaji walikuwa wakipata huduma za uchunguzi wa magonjwa kilichopo Iringa umbali
wa zaidi ya kilomita 900 kutoka Sumbawanga hali ilisababisha ugumu kwa wafugaji
na kusababisha vifo vingi vya mifugo
Hivyo Waziri Mpina
amebanisha kuwa uanzishaji wa kanda hiyo utaongeza ufanisi wa kazi ya udhibiti
wa magonjwa ya mifugo katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na kuleta ahueni
kubwa kwa wafugaji.
Mpina aliongeza kuwa hadi
sasa kuna Kanda 8 za Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo na Kanda 11 za Wakala wa
Maabara Tanzania (TVLA) ambapo wizara inakusudia kuanzisha kanda nyingine moja
katika mwaka fedha wa 2019/ 2020 itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Mara na
Shinyanga kituo hicho kikikamilika kitasogeza huduma ya udhibiti wa magonjwa
katika mikoa hiyo.
Mkurugenzi wa Huduma za
Mifugo nchini, Dk Hezron Nonga amesema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho
kumewezesha kuongezeka kwa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo na mazao
yake, shughuli za uchunguzi kimaabara zimesogezwa karibu na wananchi.
Pia upatikanaji wa chanjo
kwa wafugaji kwa bei nafuu umekuwa rahisi, kuongezeka kwa upatikanaji wa taarifa
za magonjwa , kuongezeka kwa majosho hamasa ya wafugaji kuongeza mifugo na
idadi ya lita za kuogesha mifugo.
Pia ongezeko la maduhuli ya
Serikali yatokanayo na usafirishaji wa mifugo na mazao yake ndani na nje ya
nchi kutoka makadirio ya sh milioni 120 kwa mikoa miwili Rukwa na Katavi hapo
awali na kufikia makadirio ya sh milioni 500 kwa mwaka, kufanikiwa kudhibiti
ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Dk Nonga amesema pia
kumeongezeka mahusiano kati ya wizara na Serikali za mitaa na hivyo kuongeza ufanisi
katika utoaji wa huduma za mifugo kwa wananchi tofauti na ilivyokuwa awali.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina afungua kituo cha kanda cha ufuatiliaji, utambuzi na kuzuiaiya magonjwa ya mifugo Kanda ya Kusini Magharibi Sumbawanga tarehe 30/10/2019 Mkoani Rukwa. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni