Nav bar

Ijumaa, 29 Novemba 2019

WAFUGAJI WAFURAHIA KUPATA MAENEO YA MALISHO



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ametatua changamoto ya wafugaji na wananchi wa Kata ya Mabuki katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza kwa kusimamia upatikanaji wa shamba la hekta 450 kwa ajili ya kunenepeshea mifugo.


Mhe. Ulega amesema shughuli za unenepeshaji wa ngombe unatakiwa kuanza mapema ili kuwasaidia wafugaji ambapo ametoa muda wa wiki moja kwa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kampasi ya Mabuki, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kituo cha Mabuki na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo wawe wameshaanza mchakato wa kuwapatia wafugaji maeneo hayo.


Akizungumza na wafugaji na wananchi wa Kata ya Mabuki katika ziara ya siku moja wilayani Misungwi, Mhe. Ulega amesema wafugaji wengi nchini wanapata shida ya malisho kwa mifugo yao wakati wa kiangazi, hivyo ili kuongeza thamani na kufanya ufugaji kuwa na tija wizara imekuja na njia ya kisasa ya kunenepesha mifugo wakiwemo ngombe ambapo watakuwa wanauza kwa kumpima ng’ombe uzito kwa mzani badala ya kuuza kwa makisio.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumetoa eneo la hekta 450 kwa ajili ya wafugaji wa Mabuki kunenepeshea mifugo yao kama ngombe kupitia kituo cha TALIRI Mabuki ambacho kimetoa hekta 150 huku shamba la L.M.U hekta 300, ambapo mashamba hayo yatakodishwa kwa utaratibu wa kuingiza mifugo, hivyo wananchi mzingatie kuwa maeneo hayo ni maalum kwa ajili ya kunenepeshea na atakayebainika ametoa rushwa ili kupatiwa eneo hatopata nafasi hiyo. Amesema Mhe.Ulega.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha TALIRI Mabuki Dkt. Hemel Massawe akizungumzia utaratibu wa kuingiza ngombe katika mashamba ya kunenepeshea mifugo amesema, kwa hekta moja ngombe watano ndio wanapaswa kuingizwa ambapo gharama za kukodi ni shilingi 30,000 kwa miezi 6.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Bw. Juma Sweda amesema, shamba hilo ni mali ya serikali hivyo maeneo hayo yanaweza yasitoshe kwani kuna vijiji 12 katika kata hiyo na wafugaji ni wengi na ngombe ni wengi hivyo wanahitaji kuvumiliana pia kupitia shamba hilo vijana wanapata ajira kwa kupata maziwa ya kutosha kuchakata na kuuza.


Hata hivyo baadhi ya wananchi na wafugaji wa kata hiyo akiwemo Bw. Bernard Bukumbi na Bw. Severine Masele wameishukuru ierikali kupitia wizara hiyo kwa kuwapatia shamba ambalo litawapa nafasi ya kupeleka ngombe wao kunenepeshwa.




Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akiongea kwenye mkutano wa hadhara na wanakijiji wa Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. (17/11/2019)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali wa kata, vijiji na Wilaya juu ya namna ya kuwasaidia wafugaji kupata haki zao bila kuonewa , kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhu kabla la tatizo kubwa kutokea, wakati wa mkutano wa hadhara kwenye  kijiji cha mabuki, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza. (17/11/2019)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akipokelewa kwa furaha na wanakijiji wa Mabuki, Wilayani Misungwi alipowatembelea, kusikiliza na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya kufugia Mifugo yao mkoani Mwanza. (17/11/2019)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni