Nav bar

Jumanne, 21 Agosti 2018

Wizara imejipanga kudhibiti utoroshaji wa mazao ya mifugo na uvuvi- Mhe. Ulega; Simiyu.




Utoroshwaji  wa mazao ya  Mifugo na  Uvuvi kwenda nje ya Nchi bila kibali  pamoja na matumizi ya zana haramu za uvuvi vimetajwa kuwa ni baadhi ya changamoto kubwa zinazokwamisha juhudi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kuwa sekta za Mifugo na Uvuvi  kuchangia mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega wakati wa ufunguzi wa maonesho ya nanenane kitaifa, yaliyofanyika katika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi.

Ulega alisema Wizara yake inachangia asilimia 30 tu katika uchumi wa Nchi wakati inauwezo mkubwa wa kuwekeza na kuchangia pato la Nchi kwa kiwango kikubwa.

“Mchango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika pato la Nchi ni mdogo sana ukilinganisha na sekta yenyewe, lakini sababu kubwa zinazokwamisha na kusababisha hayo ni wananchi wenyewe ambao baadhi yao wamekuwa wakitorosha mazao ya mifugo na bahari kwenda nje ya nchi bila kibali “Alisema

Alisema kwa sasa Wizara yake imejiandaa kuhakikisha wanapambana na wale wote wanatorosha mazao ya Mifugo na Uvuvi bila kibali huku wakijikita kutoa elimu na kuzuia matumizi mabaya ya zana haramu ambazo zinasababisha uzalishaji wa mazao ya bahari kupotea.

“Ni aibu sana kuona Wizara kubwa kama yangu  inachangia asilimia 30 tu katika pato la taifa…nitahakikisha tunatatua hilo kwa kufanya msako (operation ) ili kuifanya Wizara kuwa na tija…Alisema

Waziri wa Kilimo Charles Tizeba aliwataka wananchi hasa wakulima wa Mikoa ya Simiyu,  Shinyanga na Mara kuyatumia maonesho ya nanenane katika kujifunza ili yaweze kuleta tija na kubadilisha kilimo, kipato na maisha yao kwa ujumla .

Aidha alisikitishwa sana kuona sekta ya kilimo yenye nguvu kazi kubwa ya wakulima asilimia zaidi ya 70 nayo inachangia kiasi kidogo katika pato la Taifa.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka alisema kuwa maonesho hayo ya nane nane ambayo yameanzishwa kwa kanda mpya ya ziwa mashariki inayohusisha Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara yatawapunguzia wakulima kwenda nje ya nchi kujifunza .

Mtaka alisema watajitahidi kuendelea kuyafanya maonyesho hayo kuwa ni ya kimataifa na kwamba kanda hiyo itakuwa ni kitovu kikubwa kwa wakulima na wafugaji  kuja kujifunza kwa vitendo.

Kelvin Emanuel mvuvi kutoka Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inajukumu kubwa la kutoa elimu kwa wananchi juu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija badala ya kuwachomea zana zao za Uvuvi  kwani haitasaidia kutokomeza Uvuvi wa kutumia zana haramu.

binafsi naona Wizara inawajibu wa kuelimisha Uvuvi bora,  tena si tu kuelimisha bali kuelimisha na kutoa nyavu vinazotakiwa ili kwa pamoja waweze kuleta tija kwa wavuvi na Taifa kwa ujumla.



Waziri wa Kilimo Mhe. Charles Tizeba akiwa kwenye banda la Mifugo na Uvuvi, katika kiwanja cha Nyakabindi Mkoani Simiyu.



Waziri wa Kilimo akisema neno wakati akitembelea banda la Mifugo na Uvuvi katika kiwanja cha Nyakabindi Mkoani Simiyu.













Hakuna maoni:

Chapisha Maoni