Nav bar

Ijumaa, 24 Agosti 2018

KATIBU MKUU UVUVI DKT. RASHID ADAM TAMATAMAH AFANYA ZIARA WILAYANI MUSOMA.






Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya (Uvuvi) Dr. Rashid Tamatama amefanya ziara
Wilayani Musoma Mkoani Mara katika kiwanda cha samaki cha Musoma Fish Processors.

Akiongea na wafanyakazi katika kiwanda hicho, Dkt Tamatama amesema kuwa rasilimali ya uvuvi
imepungua kwa kiwango kikubwa sana kitu ambacho sio kizuri kwa mustakabali wa maisha ya baadaye. Kipato cha mwananchi mmoja mmoja kimepungua kwa kiwango kikubwa na pia kumekuwa na ulaji wa wastani wa samaki ambao ni mdogo sana kwa Watanzania. alisema.

Aidha, Katibu Mkuu Uvuvi Dkt.Tamatama alisisitiza kuwa hakuna malighafi za samaki zinazokuja kiwandani kwa ajili ya uchakataji hivyo kwa kutokuwa na malighafi hizo kunarudisha nyuma nguvu ya kufikia Tanzania ya Viwanda.

Sisi kama Wizara yenye dhamana tumeliona hilo ndio maana tumekuja na operesheni mbalimbali
ambazo zimeonyesha Mafanikio makubwa sana, kwani ukiangalia samaki waliopo viwandani na
wanaoliwa na wananchi huko mtaani ni wakubwa na wana minofu.

Hata hivyo tumepokea wazo lenu chanya la uchakataji na usindikaji wa samaki kutoka kwa Wafugaji wa Samaki wa mabwawa na vizimba. Nimekuja hapa ili tuweze kuzungumza kwa kina kuhusu maombi yenu hayo na ninaahidi kuwa Wizara itafanya utafiti kutambua kiwango cha samaki kinacho fugwa kama kitatosheleza mahitaji ya soko la walaji wa ndani na ziada kuchakatwa viwandani. Tukijiridhisha nina uhakika Wizara haitasita kutoa kibali, ninaamini mtachakata zaidi na kuongeza pato kwa Taifa. alisema.

Katika hatua nyingine, Dkt.Tamatama alisema kuwa amefurahishwa na hatua za uandaaji wa samaki
kuanzia samaki analetwa kiwandani, kuchakatwa, uhifadhi hadi kufikia kwenye hatua ya usambazaji kwenye soko la ndani na nje ya nchi. Kazi kubwa ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha tunashirikiana kupatikana kwa malighafi ya kutosha kuchakatwa kwenye viwanda na pia kuhakikisha tunafikia uchumi wa viwanda kwa kuongeza uwekezaji wa viwanda zaidi vya kuchakata na  kuongeza thamani (value addition) samaki na mazao yake .

Vilevile, Dkt Tamatamah alisisitiza na kutoa wito kwa Wavuvi na Wadau wote kuacha uvuvi haramu ili kuinua uchumi wa viwanda, na samaki wavuliwe wale wanaokidhi vigezo vya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni za Uvuvi za mwaka 2009 na sio kuvua samaki wachanga ambao bado wanahitaji kukua na kufikia umri wa kuzaa. Serikali itaendelea kuwakamata wavuvi wanaotumia zana haramu kuvua samaki kinyume cha Sheria, Kanuni na taratibu na wale wanaofanya biashara ya kuuza samaki wachanga na zana haramu.  Pia, tutaongeza nguvu zaidi na  kasi ya kupambana na uvuvi haramu hivyo ninawasihi wawekezaji wa viwanda vya samaki na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya uvuvi na biashara haramu katika Sekta ya Uvuvi.

Kwa upande mwingine, Menejimenti ya Kiwanda pamoja na baadhi ya wafanyakazi kwenye Kiwanda hicho walieleza kuwa changamoto kubwa zinazowakabili wawekezaji hao ni ugumu wa upatikanaji wa samaki ikiwa ni malighafi muhimu kwao. Hii imesababisha Wafanyakazi wengi kufukuzwa kazi,  kiwanda kimelazimika kupumguza shift za uzalishaji na kuathiri kwa kiwango kikubwa utendaji wa kiwanda,  Hali hii ndiyo sababu  kubwa ya kuomba kibali cha kuchakata samaki aina ya "Sato" kutoka kwa wafugaji samaki nchini. 

Aidha, Dr Tamatamah alieleza kuwa Wizara inatambua uwapo wa changamoto kwenye ufugaji wa samaki hususani  upatikanaji  wa vifaranga bora vya samaki kwa wingi na pia upatikanaji wa chakula bora cha samaki wanaofugwa. Akasisitiza kuwa Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi itahakikisha kwamba vifaranga vya samaki vinapatikana kwa wingi pamoja na chakula kilicho bora.

Naye Vincent Naano Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini Mkoani Mara amewaomba waliopo kwenye
sekta ya Uvuvi (agents/mawakala) waje na maandiko ili wawezeshwe kupatiwa Mikopo na TAASISI za kifedha, pia watengeneze mfumo rasmi wa ajira ili watu wanaofanya kazi ziwani wakiingia watambulike.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Bw Vicent Naano ameshauri wavuvi wadogo  wajiunge kwenye vikundi ili waweze kuwezeshwa kuendesha shughuli zao. Safari hii watakaotumia zana haramu za kuvulia hawatapigwa faini tuu, bali tutawapeleka mahakamani. alisema.


Dkt. Rashid Tamatamah akipewa maelezo juu ya mazao ya samaki yanayosafirishwa nje ya nchi.

Samaki aina ya sangara wakiwa kwenye eneo la uchakataji

Bw. George, Meneja wa kiwanda akitoa maelezo ya kiwanda.

Dkt. Rashid Tamatamah na Mkuu wa Wilaya Mhe. Vicent Naano pamoja na wajumbe wakiingia kiwandani










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni