Nav bar

Ijumaa, 20 Aprili 2018

NAIBU WAZIRI MHE. ABDALLAH ULEGA AIAMBIA KAMATI YA BUNGE KUWA SERIKALI INA MTAZAMO WA KUIFANYA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI KUWA SEKTA YA UZALISHAJI - KIGOMA


Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdalah Hamis Ulega ambaye  ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ameiambia kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji kuwa, Serikali ina mpango wa kuifanya sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
 
Naibu Waziri Hamisi Ulega ameyasema hayo leo Mkoani Kigoma mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, ilipokuwa katika ziara ya kutembelea  chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)  kampasi ya kigoma jana.
Mhe. Ulega amesema  Wizara yake ina Mkakati  wa kulinda rasilimali za Mifugo na Uvuvi, kwa kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kuitoa sekta hiyo  kwenye kuchangia kiasi na shilingi Bilioni 19 kwa  mwaka katika pato la taifa hadi kufikia kuchangia zaidi ya shilingi Bilioni 50 kwa mwaka.
“Tunaweza kufikia malengo haya kwanza kwa kuimarisha uvuvi wa Bahari kuu kwa kuhakikisha kwanza tasisi yetu ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu inakuwa na nguvu kwa kuweka vizuri sheria na kanuni zetu za uvuvi ikiwa ni pamoja na kufufua shirika letu la TAFICO, Alisema Ulega.”
Sambamba na hilo, Ulega alisema Serikali ina mkakati wa kuwa na Meli ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda kuvua na kuchakata mazao ya samaki, jambo ambalo litakwenda sambamba na ufunguaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi.
Naibu Waziri Ulega pia alisema serikali ina lengo la kuhamasisha uwekezaji katika  sekta ya Uvuvi kupitia mafunzo, utafitu na  elimu ya ugani kupitia vyuo vya Feta , ili kuweza  kuwa na wataalam wa kutosha pamoja na kuipa nguvu wakala hiyo ili kuweza  kutoa wataalam  kwani mpaka sasa sekta ya uvuvi  ina uhaba wa wataalam na kuongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa utafiti serikalii ina mkakati mkubwa wa kuweza kuiwezesha TAFIRI kwa kuipa kazi maalum za tafiti akitolea mfano wa uelewa mdogo wa baadhi ya wavuvi kuhusiana na zana halali za uvuvi.
Akizungumzia suala la kuingiza samaki aina ya vibua na sato kutoka nje ya nchi, Ulega alisema, “Ukiangalia kwa makini sioni sababu ya kwanini tutoe mathalani kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa mwaka tuwapelekee wavuvi wengine na tuingize tani  elfu 20 na zaidi kuleta hapa ndani za samaki ambao sisi wenyewe tunao.” Alisisitiza Ulega.
“ Ipo Mikakati kwa serikali ya kuwatengenezea wafanya biashara ya samaki mazingira mazuri ili pesa hiyo  iwekezwe hapa nchini.” Alisema.
Awali akitolea mfano wa ulinzi wa rasilimali za uvuvi Ulega alisema “Tumefanya ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa Victoria kwa muda mfupi tu ikiwa ni pamoja na ulinzi wa  utoroshwaji wa Mazao ya Uvuvi nje ya nchi na tumeingiza kiasi kikubwa cha fedha.” Alisema.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sekta ya Uvuvi Dkt. Yohana Budeba alisema kuwa njia ya ufugaji wa samaki wa kisasa kupitia chuo cha FETA kitatengeneza wataalam na kuongeza ajira na kupatikana samaki wengi na kupelekea mchango mkubwa wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa hili.    
Kushoto  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Hamis Ulega (Mb) akizunguma katika kikao na Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji katika chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)  kampasi ya Kigoma, kati kati ni mwenyekiti wa kamati Hiyo Mhe. Mahmoud Hassan  Mgimwa (Mb.) Kalenga na kulia ni Makamu Mwenyekiti Mhe. Christine Gabriel Ishengoma (Mb).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Hamis Ulega (Mb) kulia akiongea na Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji ilipotembelea chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)  kampasi ya Kigoma, wabunge wa kamati hiyo wameambata na maafisa mbali mbali kutoka serikalini.

Pichani Mbele ni baadhi wa wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji wakifuatilia mazungumzo katika kikao wakati wa ziara yao katika chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)  kampasi ya Kigoma.


Alhamisi, 19 Aprili 2018

MNADA WA UPILI WA PUGU KUWA MNADA WA KIMATAIFA-LUHAGA MPINA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Joelson Mpina amesema kuwa mnada wa pugu utakarabatiwa na  kuwa mnada wa kimataifa utakaokuwa unahudumia wafanyabiashara kutoka nchi yoyote Africa na duniani kwa ujumla.

Tanzania Mungu ametujalia kuwa na tunu ya Rasilimali ng'ombe,Nchi zilizoendelea wanajivunia  vitu vyao,Mfano viwanda,ifike wakati na Sisi tujivunie Rasilimali ng'ombe tuyoliyopewa Mungu Bure.

"Haiwezekani Sisi Tanzania tuwe wa pili africa kuwa na Mifugo mingi,tukitanguliwa na nchi ya Ethiopia halafu tukose kuwa  na mnada wa kimataifa"

Mpina ameyasema hayo Leo alipofanya ziara ya kukagua eneo la mnada huo lililovamiwa na wananchi na kujionea hali halisi ya uvamizi wa  eneneo hilo.

Pia baada ya kuzungu na kukagua eneo la mnada huo na kushuhudia uvamizi mkubwa uliofanyika katika eneo hilo,Mhe.Mipina ameunda timu maalumu itakayopita nyumba baada ya nyumba kuchunguza na kuhoji uhalali wao wa kuwepo katika eneo la Serikali na kujiridhisha ni nani aliyewauzia maeneo hayo wananchi hao.

Aidha Waziri Mpina amepiga marufuku ujenzi wa aina yoyote ile usifanyike katika eneo hilo mpaka hapo serikali itakapotoa ripoti ya uchunguzi huo ambapo utafanyika ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Jumla ya kaya Elfu tano (5,000) za wavamizi hao zimetambuliwa na zinakadiliwa kuwa na watu elfu 22,8000.

Vilevile baadhi ya Wafanyabiashara na wafugaji waliokuwepo mnadani hapo, wamemweleza Mhe Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuwa mnada huo unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo uchakavu wa Miundombinu ya kutunzia Mbuzi,Ukosefu wa Maji,Ubovu wa barabara iendayo mnadani hapo na uhaba wa maeneo ya kuchungia mifugo kutokana na Eneo la mnada huo kwa kiasi kikubwa kuvamiwa na wananchi.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Mifugo Dkt Maria Mashingo amesema kuwa wamefa nikiwa kuipata hati ya mnada huo baada ya kuitafuta kwa muda mrefu sana.

"Eneo la mnada wa upili wa Pugu lina ekari 1,900,kutokana na uvamizi wa eneo hilo, mnada huo kwa sasa unakadiliwa  kuwa na eneo lililobaki kwa ajili ya matumizi sahihi ya mnada ni asilimia 25 tu.Hati ya eneo la mnada huo ilitolewa mwaka 1939 na serikali ya wakati huo"Alisema

Awali Waziri Luhaga Mpina alifika mnadani hapo majira ya saa kumi alfajiri akiambatana na Katibu Mkuu Mifugo Dkt. Maria Mashingo na baadhi ya Maafisa kutoka Wizarani.Kazi ya kwanza aliyoanza nayo mara tu baada ya kufika mnadani hapo ni kukagua Vibali (Movement Permit) katika makundi ya ng'ombe yote yalikuwepo kwa wakati huo.

Waziri mpina akiwa katika mnada wa Mbuzi Pugu alifanikiwa kumkamata mfanyabiashara mmoja wa Mbuzi aliyejulika kwa  jina la Zacharia Mabula (43) aliyekwepa kulipia ushuru wa Mbuzi 112 kati ya Mbuzi 228 aliokuwa nao.Kwa kutumia sheria taratibu na kanuni zinazoendesha mnada huo,mfanyabiashara huyo amepigwa faini ya Tsh.800,000/=

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Luhaga Mpina kushoto akiwa na Katibu Mkuu Mifugo Dkt. Maria Mashingo wakiangalia malisho ya ng'ombe katika mnada wa Pugu

Mhe. Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia mbuzi alipotembelea mnada wa Pugu ivi karibuni.

Mhe. Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia ng'ombe akiwa mnadani

WAZIRI MPINA APOKEA MADUME 11 YA NG'OMBE BORA KATIKA KITUO CHA NAIC - ARUSHA

Mhe.Waziri Luhaga Mpina akiwa na Katibu Mkuu Mifugo Dkt. Maria Mashingo akikata utepe kuashiria kupokelewa kwa Madume hayo ya Mbegu


Maelekezo ya Mhe. Waziri wakati alipokuwa akipokea madume ya ng'ombe bora 11 ya mbegu katika Kituo cha Uzalishaji Mifugo kwa Chupa (NAIC) Arusha.

1.Amemshukuru na kumpongeza KMM kwa kazi kubwa ya kuhakikisha utoshelevu wa mbegu za AI kwa kuwepo kwa jumla ya madume bora 26 hadi sasa yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya dozi 3,120,000 kwa mwaka.

2.Amemuagiza KMM kuandaa mpango maalum wa kuhimilisha Ng'ombe Milioni moja wa maziwa.Mpango huo uanze kutekelezwa katika bajeti ya mwaka huu(2018/19). 

3.Pia Mhe. Waziri amemuagiza KMM kufanya tathmini ya kuona kama kuna haja  au umuhimu wa kuagiza maziwa na mazao yake nje ya nchi.Tathimini hiyo inatakiwa kukamilika katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa. 

4.Aidha Mhe. Waziri amemuagiza KMM  kufanya tathmini ya kuona kama maziwa na mazao yake yanayoingizwa nchini yanaingia kwa kufuata taratibu zote za kisheria. Tathmini hiyo  pia ifanyike ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

5.Mhe. Waziri ameonya wafanyabiashara wote Wanaoingiza bidhaa za maziwa na mazao yake kwa njia za magendo, kuacha mara moja.Serikali itafanya ukaguzi na itachukua hatua kali za kisheria kwa mfanyabiashara yoyote atakayebainika.

WANAOAGIZA NYAMA, MAZIWA NA SAMAKI KUTOKA NJE YA NCHI SIKU ZAO ZAHESABIKA - ULEGA KIGOMA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega, amesema kuwa wanaoagiza nyama, maziwa na samaki kutoka nje ya nchi, siku zao zahesabika kutokana na nchi kuwa na mifugo ya kutosha kama vile Ngombe, Mbuzi, Kondoo, Kuku na Punda. Hivyo, Taifa kama Tanzania halina sababu yoyote ya kuagiza mazao hayo ya mifugo na uvuvi kutoka nje ya nchi.
Naibu waziri Ulega aliyasema hayo alipokuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani Kigoma ya kutembelea Mwalo wa Samaki wa Muyobozi Uliyopo Wilayani Uvinza na Mwalo wa Kibirizi na kituo cha Taasisi ya Tafiti za Uvuvi Tanzania TAFIRI Kigoma.
“Sioni kwanini tuagize nyama na maziwa  toka nje  ya nchi, hatuwezi kuendelea kuangiza nyama, maziwa na hata mazao ya uvuvi, kwa nini tusiwekeze katika rasilimali zetu za ndani  katika mifugo na samaki na kuongeza pato la taifa? “Aliuliza Ulega.
Ulega  aliongeza kwa kusema kuwa Wizara yake haitawavumilia  wafanyabiashara wanaoagiza nyama, maziwa na mazao ya samaki  toka nje ya nchi kwani sekta ya mifugo na uvuvi ni sekta ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuleta tija katika taifa.
Tarkibani “tani elfu 20 za samaki zinaingizwa kutoka nje ya nchi kila mwaka, samaki ambao wanafugwa katika maeneo mengine duniani, lakini sisi hapa nchini tunao katika mazingira ya asili.” Alisema
 Na hapa Mhe. Ulega aliitaka TAFIRI kuhakikisha wanawafikia wafugaji wa samaki kwa kufanya tafiti zao ili kujua changamoto wanazokutana nazo na kujua namna ya kuzitatua, akitolea mfano wa chakula sahihi kinachotakiwa kupewa masamki wanaofugwa na kuangalia miundombinu ya kufugia.
Akizungumzia suala la zana za uvuvi katika ziwa Tanganyika alipokuwa akiongea na watafiti na watumishi wa TAFIRI, Ulega alisema “TAFIRI mfanye tafiti ya aina ya nyavu zinazotumiwa kwa kiasi kikubwa na wavuvi  ili kuona kama zinafaa kuendelea kutumika, maana kumekuwa na malalamiko toka kwa wavuvi yanayopelekea kushuka kwa kiwango cha upatikanaji wa samaki na dagaa katika ziwa hili kutokana na matumizi ya nyavu hizo.” Alisema
Sambamba na hilo Ulega alisema Wizara yake ina mpango wa kuimarisha eneo la tafiti kwa kuongeza rasilimali fedha kwa kukarabati miundombinu na kuongeza rasilimali watu.
“Kila Mwaka TAFIRI itakuwa inafanya tafiti kuhusu mambo ambayo Wizara itakuwa imeyaelekeza ili kuondokana na suala la watafiti hawa kufanya kazi za watu wengine.” Alisema
Akizungumzia swala la mafanikio ya soko la nyama la nje ya nchi, Ulega alisema, “Hatuwezi kusafirisha nyama nje ya nchi kama mkakati wetu wa chanjo ya mifugo hauko sawa, lazima tuwe na mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo, soko la kimataifa linaangalia sana swala hili, Sisi kama Wizara tunaenda kusema kuwa kwa yoyote anayetaka kufuga swala la chanjo ni lazima.” Alisisiza Ulega.
Ulega aliendelea kusema kuwa ni lazima wizara kutengeneza mikakati ambayo itamfanya mfugaji asitaabike wazo wambalo amesema kama litaridhiwa litafanyiwa kazi.
“kuna watu wanaona mifugo ni balaa, mifugo siyo balaa mifugo ni neema.” Alisisitiza.
Aidha Ulega alisisitiza suala la uwekezaji kwa ufugaji wa samaki kama njia ya kusaidia kupunguza kiwango kikubwa cha uvuvi haramu wa samaki katika maeneo mbalimbali nchini, huku akipongeza jitihada za taasisi ya utafiti wa samaki TAFIRI kushirikiana na wananchi na kuonesha mfano wa namna ya ufugaji bora wa samaki unaowaonesha wafugaji wa samaki kuitumia ili kufikia malengo waliyokusudia.
Naibu Waziri Ulega pia alisema Serikali imepanga kuongeza makusanyo katika sekta ya mifugo kutoka bilioni kumi na sita hadi bilioni hamsini baada ya kuifanya mifugo ya ndani kuwa bora na kuwa ya kiushindani katika soko la kimataifa, hivyo suala la chanjo litakuwa la lazima.
Kulia Dkt. Emmanuel Sweke Kaimu Mkurugenzi wa kituo wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa  Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma,  akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega aliyekaa katikati  wakiwa katika boat wakielekea kuangalia kizimba cha kufugia samaki katika maji ya ziwa Tanganyika, kushoto ni Afisa Mifugo wa Mkoa wa Kigoma Bw. Noel Byamungu.

Kushoto Dkt. Emmanuel Sweke, Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma akimuonyesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega katikati, kizimba cha kufugia samaki kilichopo katika maji ya ziwa Tanganyika hakipo pichani, alipotembelea kituo hicho mjini kigoma jana. Kulia ni Afisa Mifugo wa Mkoa Bw. Noel Byamungu.

Aliyesimama ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega, akiongea na watumishi wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa  Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma, pamoja na watafiti hawapo pichani, alipotembelea kituo hicho, kulia ni Dkt Emmanuel Sweke, Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, na kushoto ni  Mkurugenzi wa tafiti na mafunzo katika chuo cha mafunzo ya uvuvi  FETA Kigoma, Bw. Simtie Ambakisye.