|
Mhe. Dkt. Charles Tizeba |
HOTUBA
YA WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI MHE, MHANDISI, DKT. CHARLES JOHN TIZEBA (MB)
WAKATI WA KUMKARIBISHA MGENI RASMI KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKUKUU YA
WAKULIMA, NANE NANE KITAIFA, VIWANJA VYA NGONGO KATIKA MANISPAA YA LINDI TAREHE
8/8/2017
Mheshimiwa,
Mgeni Rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Waheshimiwa
Mawaziri wa Tanzania Bara na Visiwani,
Makatibu
Wakuu wa Tanzania Bara na Visiwani,
Waheshimiwa
Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara,
Makatibu
Tawala wa Mikoa,
Mhe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji
Waheshimiwa
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa
Wakuu wa Wilaya,
Waheshimiwa
Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri mliopo,
Wakurugenzi
wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji,
Wataalamu
wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ushirika,
Wanahabari
wa Vyombo mbalimbali,
Wageni
Waalikwa,
Mabibi
na Mabwana,
Kwanza
kabisa, naomba kuchukua fursa hii kukushukuru, Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kufika na kushirikiana na Wakulima, Wafugaji
na Wavuvi katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Wakulima, Nane Nane, yanayohitimishwa
leo, hapa katika Viwanja vya Ngongo katika Manispaa ya Lindi na kwenye Kanda
nyengine.
Kufika
kwako, kwa mara ya pili mfululizo kwenye maadhimisho yetu kunadhihirisha jinsi
unavyotilia maanani umuhimu wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, hususan katika
maendeleo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Napenda pia kwa niaba ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, nikushukuru sana kwa
jinsi ulivyotenga muda wako na kutembelea mabanda ili kuona hali halisi ya Maadhimisho
pamoja na teknolojia za uzalishaji, na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kama
ambavyo umeona na kusikiliza, waoneshaji na waandaji wa Maadhimisho haya, Sekta
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa muda mrefu zitaendelea kuwa muhimili na
kichocheo katika kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio kipaumbele cha Serikali
ya Awamu ya Tano unayoiongoza. Naomba, nikuhakikishie kuwa, Mimi na Watumishi katika
Wizara yangu, tumejipanga kuhakikisha kuwa, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
inaendelea kukua sawa sawa na mahitaji ya Wananchi. Hilo linawezekana na tutaweza
kuzalisha malighafi za kutosha za kuwezesha viwanda kuzalisha bidhaa mbalimbali,
ambazo zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa bei nzuri na ya ushindani. Hivyo ndivyo
tutaweza kuongeza mchango wa Sekta hizi katika uchumi wa Taifa na pia katika
kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi.
Mheshimiwa Mgeni rasmi,
Sekta
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko
ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na
tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji. Tumejipanga kuendelea, kukabiliana na changamoto
za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora
zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi.
Napenda
pia kutoa taarifa kuwa, Serikali yako kwa kushirikiana na Wabia wa Maendeleo, tumekamilisha
Mpango wa Kilimo Kinachohimili Mabaliliko ya Tabianchi na Miongozi ya
uzalishaji mazao, ufugaji na uvuvi. Muongozo wa kilimo umetolewa kulingana na Kanda
za Kilimo za Kiteknolojia. Miongozo hiyo, imezinduliwa na kuanza kusambazwa kwa
Maafisa Ugani wa Kilimo Mifugo na Uvuvi na kwa wananchi, kuanzia Mwezi, Mei na
Juni, 2017.
Mikakati
mingine, tunayoendelea nayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa mbolea bora, inapatikana
kwa wingi na kwa bei nafuu zaidi, sawasawa na agizo lako la kuwasaidia
Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kupunguza gharama za uzalishaji ili waweze kufaidika
na matunda ya juhudi zao.
Sambamba
na hilo, tumepanga na tutahakikisha kuwa tunaendelea kuwaelimisha na kuwasaidia
Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalam zaidi ili kuepuka hali ya kuhamahama kwa ajili
ya kutafuta malisho na maji.
Hilo,
litatuwezesha kufuga kwa tija na pia kupunguza migogoro ya Wakulima na Wafugaji.
Napenda
pia kukuhakikishia kuwa, tumedhamiria kuboresha zaidi Sekta ya Uvuvi ili
kuongeza uzalishaji na tija, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake katika
pato la Taifa. Hapa tutahamasisha watu wengi kufuga samaki katika mabwawa na
vizimba ili tuweze kuzalisha samaki wengi zaidi sambamba na kuboresha zaidi uvuvi
wenye tija na ambao ni endelevu. Niishukuru sana Ofisi yako Mhe. Makamu wa Rais
kwa hatua inazozichukua kulinda mazingira ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja na
kurahisisha upatikanaji wa cheti ya kukidhi matakwa ya utunzaji mazingira.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mipango
tuliyojiwekea, tutaitekeleza kwa ufanisi zaidi kwa kuhimiza ushiriki wa Sekta
Binafsi, kuwekeza zaidi katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuzingatia mnyororo
wa thamani ili kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa nchi yenye
uchumi wa kati ifikapo au kabla ya mwaka 2025.
Hili linaendana na Kaulimbiu ya mwaka huu, inayosema;
“Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo
Mifugo na Uvuvi ili kufikia uchumi wa kati”
Kupitia
Kaulimbiu hii tunahimiza, matumizi ya nyenzo sahihi kama matrekta, na mashine
nyingine za uzalishaji na usindikaji, kuongeza uwekezaji katika viwanda vodogo,
vya kati na vikubwa, sambamba na kuweka mazingira bora yanayovutia Sekta
Binafsi kuwekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia mnyororo wa thamani. Katika
Maadhimisho haya, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine
wamepata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili hatmae Sekta hii iweze
kuongeza uzalishaji na tija zaidi.
Kwa
kuongeza uzalishaji, tutajihakikishia ziada kubwa ya chakula na malighafi za
kutosha katika viwanda vilivyopo na vinavyotarajia kuanzishwa. Kama ambavyo,
tunafahamu kuwa upatikanaji wa masoko ya uhakika, utachochea zaidi uzalishaji
wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, uhakika wa bei kwa mazao na bidhaa
zinazozalishwa na Mkulima, Mfugaji na Mvuvi atakayewekeza zaidi katika
uzalishaji.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mwisho,
napenda pia, kukupongeza, Mhe. Rais kwa jitihada unazozichukuwa, pamoja na Serikali
unayoiongoza katika kudhibiti matumizi, kuongeza makusanyo, kuhamasisha ujenzi
wa viwanda, kulinda maliasili zetu, hususan madini na rasilimali zingine ili
Taifa letu, liweze kufaidika, kupitia rasilimali hizo. Kwa niaba ya Wakulima,
Wafugaji na Wavuvi.
Aidha,
napenda kutoa shukrani kwako, na kwa Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa
kukubali kuondoa na kupunguza baadhi ya tozo, ushuru na kodi ambazo zilikuwa
kero kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Naomba nikuahidi kuwa, Wizara ya Kilimo Mifugo
na Uvuvi, itaendelea kusimamia maagizo unayotoa ili kuleta faraja kubwa kwa
Wakulima, Wafugaji na Wavuvi na kuhamasisha Sekta Binafsi kuongeza uwekezaji
katika Sekta hizo.
Baada
ya kusema hayo, naomba sasa, nikukaribishe ili uongee na Watanzania kupitia
hadhara hii.
Mheshimia Rais, Karibu sana!