Na Hamis Hussein, Zanzibar
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea Meli ya Utafiti wa Uvuvi kutoka Nchini Norway kwa lengo la kufanya utafiti wa wingi wa Rasilimali za Uvuvi na Mfumo wa Ikolojia.
Akizungumzia ujio wa Meli hiyo Wakati wa Mapokezi yaliyofanyika Leo Aprili 02, 2025 katika Bandari ya Malindi Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluuu Zanzibar, Mhe. Shaaban Ali Othman amesema Meli hiyo ijulikanayo kwa jina la Dr. Fridjof Nansen itaisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujua uelekeo mpya wa Sekta ya uchumi wa Buluu na kuwasaidia wavuvi kujua maeneo ambayo samaki wanapatikana kwa uhakika.
"Ujio wa Meli hii kwetu sisi kama Tanzania na kama Zanzibar inatusaidia kujua uhalisia wa rasimali za uvuvi zilizomo katika Bahari yetu, Serikali imeshafanya uwekezaji mkubwa kupitia baharini, kwahiyo taarifa za kitaalam na takwimu zitazopatikana zitawasaidia pia wavuvi wetu" alisema Mhe. Shaabani Ali Othman.
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali itaendelea kusimamia tafiti zinazofanywa na wataalam kuhusu rasilimali za baharini ili zijikite kwenye kujua wingi wa rasilimali za uvuvi zinazopatikana kwenye Bahari.
"Tutafurahi kuona utafiti uliopita ulionyesha kulikuwa na ongezeko la rasilimali tulizonazo ndani ya maji yetu lakini tunahimiza utafiti utakaofanyika awamu inayofuata mwezi Oktoba ujikite katika kujua wingi wa rasilimali tulizonazo kwenye Bahari yetu" alisema Dkt. Mhede.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), DKt. Ismael Kimirei amesema utafiti wa awamu hii unaoanza kufanyika Alhamisi ya Aprili 03, 2025 utaanzia kwenye maji ya Bahari ya Hindi upande wa Kusini mwa Mtwara hadi mwisho wa Pemba huku ukitarajiwa kutumia Siku 19 kwa kukusanya taarifa za wingi wa Samaki, mtawanyiko wake na aina mpya za Samaki zitakazopatika.
Aidha, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO Nchini Tanzania Dkt. Nyabenyi Tipo amewahimiza wadau kushirikiana na Serikali kufanya mijadala ya kuimarisha uhai wa Viumbe maji vinavyopatika kwenye Bahari ya Hindi ili viweze kuinua Uchumi wa buluu na maisha ya Wavuvi kwa ujumla.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi- Zanzibar Mhe. Shaaban Ali Othman (Katikati, Waliokaa), akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara za Mifugo na Uvuvi (JMT) na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi (SMZ), Mkurugenzi Mkazi wa FAO-Tanzania na watafiti mbalimbali mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ndani ya meli eneo la Bandari ya Malindi, ikiyopo Mjini Unguja, Zanzibar Aprili 02, 2025.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi-Zanzibar Mhe. Shaaban Ali Othman akizungumza wakati wa mapokezi ya Meli ya Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi Baharini iitwayo Dr. Dr. Fridtjof Nansen, Hafla iliyofanyika Bandari ya Malindi Mjini Unguja, Zanzibar, Aprili 2, 2025.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe akielezea jinsi serikali ya Tanzania itakavyoendelea kusimamia Tafiti za Uvuvi wakati wa mapokezi ya Meli ya Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi Baharini inayojulikana kama Dr. Fridtjof Nanseni. Hafla ya mapokezi ya meli hiyo imefanyika katika Bandari ya Malindi Mjini Unguja, Zanzibar, Aprili 2, 2025.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi -Zanzibar Mhe. Shaaban Ali Othman (Watatu Kushoto ) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtafiti wa Meli ya Utafiti ya Dr. Fridtjof Nansen wakati alitembelea maeneo mbalimbali ndani ya meli hiyo ili kujifunza namna utafiti unavyofanyika kwa kutumia vifaa vya kisasa., Hafla ya mapokezi ya meli hiyo imefanyika katika Bandari ya Malindi Mjini Unguja, Zanzibar, Aprili 2, 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania Dkt. Ismael Kimirei akizungumzia juu ya Tafiti za Viumbe maji wa baharini na tija itakayopatikana katika kuimarisha uchumi wa Buluu wakati wa mapokezi ya Meli ya Utafiti ya Dr. Fridjof Nansen hafla iliyofanyika Bandari ya Malindi, Mjini Unguja, Zanzibar Aprili 02, 2025.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kikimo Duniani FAO Nchini Tanzania Dkt. Nyabeti Tipo akizungumza wakati wa mapokezi ya Meli ya Utafiti ya Dr. Fridtjof Nanseni, Hafla iliyofanyika Bandari ya Malindi Mjini Unguja, Zanzibar, Aprili 2, 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI) Dkt. Zakaria Hamis akitoa neno la Ufunguzi katika hafla ya kupokea Meli ya Utafiti ya Dr. Fridjof Nansen. Hafla hiyo, imefanyikakatika Bandari ya Malindi, Mjini Unguja, Zanzibar Aprili 02, 2025.
Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Shekh akitoa neno la Shukran kwa Shirika la FAO, Serikali ya Norway kwa kuwezesha ujio wa Meli ya Utafiti ya Dr. Fridjof Nansen Wakati wa Hafla ya Mapokezi ya Meli hiyo iliyofanyika Bandari ya Malindi, Mjini Unguja, Zanzibar Aprili 02, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni