Na. Mbaraka Kambona, Mwanza
Wadau wa sekta ya uvuvi
kutoka Kanda ya Ziwa Victoria wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi adhimu wa mkopo wa
masharti nafuu wa maboti na vizimba wakiamini kuwa mradi huo ndio umebeba mustakabali
mwema wa sekta ya uvuvi hapa nchini.
Wamesema mradi huo ambao ni
wa kwanza kutekelezwa hapa nchini na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan unaleta
matumaini makubwa kwao kwani sasa wataweza kufanya shughuli zao za uvuvi kisasa
na kusaidia kuboresha mnyororo mzima wa mazao ya uvuvi.
Sehemu ya wadau hao wa
uvuvi kutoka Kanda ya Ziwa Viktoria wakiongea kwa nyakati tofauti wakiwa mkoani
Mwanza hivi karibuni wameeleza hisia zao na maoni mbalimbali juu ya hatua hiyo
ya Rais samia kuwakopesha boti na vizimba.
Mwenyekiti wa Chama Cha
Ushirika Cha Wauza Samaki Mwaloni (USAMWA),Mwanza, Bw. Erasto Barosha amempongeza Rais, Dkt.
Samia kwa kuwaletea mradi huo wa kuwakopesha wavuvi vizimba na maboti akisema
kuwa unakwenda moja kwa moja kuwagusa na kuwainua wananchi wa hali ya chini.
Ameongeza kwa kusema kuwa
kwa muda mrefu ziwa hilo hawakuwa wakilitumia vizuri lakini kupitia mpango huo
wa Rais Samia sasa wanakwenda kutumia ziwa hilo vizuri huku akiamini kuwa mradi
huo unakwenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye uchumi wa buluu.
Katibu wa Ushirika wa
Wachakata Samaki (UWASA), Bw. Shabani Hamisi amemshukuru Rais Samia kwa kupata
wahyi wa kuwainua watu wa chini kwa kuwaletea zana bora za uvuvi.
“Hapa Rais wetu ametumia
falsafa; mtu usimpe samaki, mpe ndoano akavue…sasa hapa ameamua kutukabidhi
ndoano tukavue ili tutoke katika hali ya chini na kuinua kipato chetu”, amesema
“Nimuahidi Rais wetu,
hatutamuangusha, tutafanya vizuri zaidi ili hata kama ana kingine cha kutupa
asisite kutuletea”, ameongeza
Naye, Katibu wa Chama Cha
Ushiriki Cha Wauza Samaki Tushirikiane (WASATU), Bw. Luka Katabalo amempongeza
Mhe. Rais kwa niaba ya wanachama wa
(WASATU) mkoani Mwanza huku akisema kuwa mradi huo utasaidia kutoa ajira nyingi
zaidi na kuinua kipato cha wanaushirika na taifa kwa ujumla.
Aidha, ametumia fursa hiyo
pia kumshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kwa kusimamia
vizuri sekta na kuwajali vyama vya ushirika.
“Mhe. Ulega wakati wote
amekuwa akitusikiliza katika shughuli zetu hizi na tunamuomba asituchoke
aendelee kutuunga mkono ili sekta hii ya uvuvi iendelee kuleta tija zaidi hapa
nchini”, amesema
Mfanyabiashara wa Mazao ya
Samaki katika Mwalo wa Kilumba jijini Mwanza, Bw. Jonas Luvanga amesema kuwa
mradi huo umekuja wakati muafaka kwani wavuvi wengi wanachangamoto ya mitaji
hivyo mradi huo wa mkopo wa maboti kwa wavuvi unaleta suluhisho la changamoto
hiyo.
“Kwa kutupatia maboti ya
uvuvi yatatusaidia kuboresha uchumi wetu sisi kama wananchi na taifa kwa
ujumla, Ahsante sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan”, alibainisha
Kwa Upande wake, Mvuvi wa
Ziwa Victoria, Bw. Gerald Mayala amesema mradi huo utakuwa na faida kubwa kwao.
Mradi huu utatusaidia kuondokana na uvuvi wa mazoea na utasaidia sana kupunguza
uvuvi haramu kupitia ufugaji wa vizimba
Mfanyabiashara wa Samaki
katika Mwalo wa Kilumba, Bw. William Clemence amesema kuwa anaamini mradi huo
wa maboti na vizimba utawasaidia kupata mazao mengi ya uvuvi ambayo wataweza
kuuza nje ya nchi kama vile Kongo na kuweza kukuza kipato chao na nchi kwa
ujumla wake.
Januari 30, 2024, Mhe.
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kugawa maboti 55 na Vizimba 222 kwa
wavuvi wa Kanda ya Ziwa Viktoria tukio ambalo litafanyika katika uwanja wa
Nyamagana jijini Mwanza ambapo pia ataongea na Wananchi kupitia tukio hilo.
Wafanyabiashara wa samaki
katika soko la Kirumba, jijini Mwanza wakipima samaki aina ya sangara katika
mzani kabla ya kuwachakata na kuwauza katika masoko mbalimbali ya ndani na nje
ya nchi.
Mmoja wa Wafanyabiashara wa
Samaki katika Soko la Kirumba, jijini Mwanza akionesha samaki aina ya Sangara
wanaopatikana katika ziwa victoria ambao wanawakausha na kuwauza nje ya nchi
ikiwemo Kongo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni