Nav bar

Jumatano, 6 Septemba 2023

KUPITIA AGRF 2023 TUTAUZA PROTINI KWA NCHI ZENYE MAHITAJI-ULEGA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Wizara yake itatumia Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula (AGRF) kuitangazia dunia dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha na kuuza kwa wingi Protini itokanayo na mazao ya Mifugo na Uvuvi..


Mhe. Ulega amebainisha hayo Septemba 05, 2023 wakati wa mahojiano yake na vyombo vya habari kwenye viunga vya ukumbi wa JNICC jijini Dar-es-salaam kunakofanyika mkutano huo ambapo amesema kuwa kwa kuanzia Wizara yake imeona fursa ya soko la mayai  kwenye nchi zenye mahitaji makubwa ya chakula. 


“Tunafahamu kwa sasa mashirika ya kimataifa  yamekuwa yakipeleka mazao ya nafaka kwenye nchi hizo kwa hiyo na sisi tumeiona fursa ya kupeleka mazao yatakayoongeza protini ambapo tunataka sasa wafugaji wetu waongeze kiwango cha uzalishaji wa mayai na ikiwezekana tuyachemshe kabisa ili kuyaongezea thamani na kuyapeleka huko” Amesema Mhe. Ulega.


Me. Ulega ameongeza kuwa kwa sasa nguvu kubwa ya uzalishaji imeelekezwa kwa wanawake na vijana ambapo amebainisha kuwa anaamini kama kundi hilo likiwezeshwa mtaji ya kutosha na teknolojia ya kisasa litaongeza kasi ya uzalishaji wa mazao yote yatokanayo na sekta ya Mifugo na Uvuvi na hivyo kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.


Mkutano wa Jukwaa la kimataifa la mifumo ya chakula (AGRF) utafanyika kuanzia septemba 05-08, 2023 ambapo mada mbalimbali zinazolenga kuboresha uzalishaji na masoko ya mazao yatokanayo na sekta ya kilimo kwa ujumla zitawasilishwa, kujadiliwa na kufikiwa maamuzi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia), Waziri wa Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (katikati) na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe wakifurahia jambo muda mfupi baada ya kukamilika kwa jukwaa la majadiliano ya Sekta ya  Kilimo ikiwa ni sehemu ya matukio yaliyofanyika kwenye Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula (AGRF) Septemba 05, 2023 jijini Dar-es-Salaam.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na viongozi wengine wakifuatilia video fupi ya shughuli mbalimbali za sekta ya kilimo wakati wa jukwaa la majadiliano ya sekta hiyo lililofanyika Septemba 05, 2023 kwenye moja ya kumbi za JNICC kunakofanyika Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula  mwaka huu (AGRF 2023).

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdul Majid Nsekela wakifurahia jambo kwenye viunga vya JNICC jijini Dar-es-Salaam kunakofanyika Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula (AGRF) mwaka 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akimtambulisha Mkurugenzi wa kampuni ya uzalishaji malisho kwa kutumia teknolojia ya kisasa (JEAA) Bw. Adam Owango kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kusindika maziwa ya ASAS Bw. Fuad Abdi (katikati) kwenye viunga vya ukumbi wa JNICC jijini Dar-es-salaam kunakofanyika Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula Septemba 05, 2023.

#MifugoNaUvuviNiUtajiri

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni