Nav bar

Jumapili, 10 Septemba 2023

EMEDO YAWAPIGA MSASA WANAHABARI

Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari wamepatiwa mafunzo kuhusu Mradi wa Kuzuia Kuzama Maji (wavuvi) – Ziwa Victoia unaoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo ya Uchumi (EMEDO).

 

Akifungua warsha hiyo Mjumbe wa Bodi ya EMEDO, Edwin Soko amesema lengo la kukutana na wanahabari ni kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu shughuli zinazofanywa na shirika hilo pamoja na kazi zitakazofanyika kwenye Mradi wa Kitaifa wa Kuzuia Kuzama Maji – Ziwa Victoria.

 

Soko amesema wanahabari wanalojukumu kubwa la kihakikisha wanauelezea umma wa watanzania juu ya umuhimu wa kujikinga na tatizo la kuzama maji. Uzamaji maji umekuwa ukitokea katika maeneo mbalimbali lakini bado elimu ya kutosha haijatolewa kwa jamii kuhusu kujikinga pamoja na madhara yake.

 

Wanahabari wamesisitizwa kuandika habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za mradi huo wa kuzuia kuzama maji kwa kuzingatia weledi na maadili ya uandishi wa habari kwani kwa kufanya hivyo wataweza kusaidia kufikisha elimu na uelewa kwa wananchi na hivyo kuwa sehemu ya wadau muhimu wa EMEDO katika kupunguza tatizo la uzamaji maji Tanzania.

 

Aidha, licha ya wanahabari kusisitizwa kuandika habari zinazoelezea utekelezwaji wa mradi huo, pia wametakiwa kuandika habari zenye kuleta mabadiliko ambazo zitasaidia kutoa elimu na majibu ya namna ya namna ya kupunguza tatizo la kuzama maji hapa nchini.

 

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Mradi huo wa kuzuia kuzama maji unaotekelezwa na EMEDO kwenye Ziwa Victoria, Meneja Mradi, Arthur Mugena amesema kuwa baada ya kufanya utafiti wa ukubwa wa tatizo la kuzama maji kwenye maeneo ya Goziba na Mulumo (Muleba – Kagera), Sweya, Buzegwe na Musozi (Mwanza), na Busekera na Kome (Mara) iliwalazimu kuanzisha mradi wa huo mwaka 2022 ambao kwa awamu ya kwanza utatekelezwa mpaka mwaka 2025.

 

Katika utafiti uliofanyika baadhi ya changamoto walizozibaini ni pamoja na ujuzi mdogo wa mbinu za kuogelea, vyombo duni na matengenezo ya boti yasiyozingatia ubora, ujuzi mdogo wa matumizi ya boti.

 

Mugena amesema Mradi huo umenza kutekelezwa kwenye maeneo saba ambayo yalitumika kufanyiwa tafiti. Walengwa wa mradi huo ni wavuvi wadogo, bodaboda (vijana wanaotumika kuegesha mitumbwi), wanawake katika mnyororo wa thamani wa samaki na Watoto kwa kuwa hao ndio wameonekana kuwa kwenye hatari kubwa ya tatizo la kuzama maji kwenye Ziwa Victoria.

 

Lengo la utekelezwaji wa mradi huo ni kuhakikisha wadau wote wa sekta ya uvuvi wanashirikiana kuhakikisha hatua za kuzuia tatizo la kuzama maji kwenye Ziwa Victoria linapungua kama sio kumalizika. Na katika kutekeleza hilo EMEDO imekuwa ikishirikiana na Serikali, Wanahabari na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 

Mugena amesema kuwa kazi kubwa zinazokwenda kutekelezwa kwenye Mradi wa Kuzuia Kuzama Maji ni pamoja na Ufahamu na ujuzi wa usalama wa maji, usimamizi wa taratibu za uvuvi, utoaji na matumizi ya taarifa za utabiri wa hali ya hewa, uchukuaji wa hatua za dharura pale linapotokea tatizo, ushirikishwaji wa jamii katika utekelezaji na kuizungumzia jamii kuhusu namna bora za kupunguza au kuzuia kuzama maji.

 

Katika warsha hiyo, wanahabari walipata fursa ya kujadili kwa kina kuhusu kazi zinazokwenda kutekelezwa na mradi kwa lengo la kupata uelewa ili waweze kuandika taarifa za mradi kwa usahihi. Aidha, wanahabari hao kwa pamoja wamekubaliana kuandika habari kuhusu shughuli zinazotekelezwa na mradi kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na tatizo la kuzama maji.

 

EMEDO ni shirika lisilo la kiserikali la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo ya Uchumi ambalo limeanza kutekeleza shughuli zake mwaka 2006 na makao makuu yake yapo Jijini Mwanza. Shirika hili linajishughulisha na Sekta ya Mazingira na Sekta ya Uvuvi ambapo linawagusa wavuvi wadogo (kwa kuangalia usalama na mazingira ya uvuvi) na uwezeshaji kiuchumi kwa kuzingatia wanawake na jinsia.

 

Utekelezaji wa mradi wa kuzuia kuzama maji utakuwa shirikishi, mafunzo kwa BMU, wavuvi na hata maafisa uvuvi wanaofanya kazi kwenye maeneo ya mradi yatatolewa kwa kushirikiana na taasisi za serikali zilizo na mamlaka ya kutoa mafunzo mbalimbali mfano wataalamu kutoka Jeshi la zima moto na uokoaji, FETA, maafisa uvuvi waliobobea katika masuala ya miongozo ya Vikundi vya Usimamizi Shirikishi vya Rasilimali za Uvuvi (BMU)  na taasisi zingine kulingana na mahitaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni