Nav bar

Jumapili, 11 Juni 2023

MWANI YAWA LULU MKOANI LINDI

Zao la Mwani limeanza kukimbiliwa na wananchi wengi wa mkoa wa Lindi kutokana na kuongezeka kwa bei ya zao hilo sokoni kadri siku zinavyokwenda.


Hilo limedhihirishwa na baadhi ya wakulima wa zao hilo kutoka vijiji vya Nachunyu, Mmumbu, Shuka na Sudi  walipotoa ushuhuda huo mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyofika Wilayani Mtama Juni 7, 2023  kwa lengo la kutoa mafunzo na elimu kuhusu mkopo usio na riba wa pembejeo za zao la mwani unaoendelea kutolewa na Serikali ya awamu ya 6 kwa wakulima hao.


Mmoja wa wakulima hao Bi. Fatuma Bakari amesema kwa hivi sasa ana uwezo wa kuvuna mpaka kilo 600 kwa mwezi ambazo humuingizia zaidi ya shilingi 1,300,000 faida ambayo imemwezesha kujenga nyumba ya kisasa na kusomesha watoto wake huku mmoja akitarajiwa kujiunga na elimu ya juu.


Naye Shabani Ally kutoka kijiji cha Sudi amesema kuwa baada ya kuona biashara ya zao la mwani inalipa aliamua kuachana na shughuli ya uvuvi aliyokuwa akifanya hapo awali na kujiunga na kikundi cha kilimo cha zao hilo ambacho kimewawezesha kuwa na uwezo wa kuvuna hadi kilo 200 kwa mwezi huku wakitarajia mavuno makubwa zaidi baada ya kuwezeshwa mikopo isiyo na riba ya pembejeo za zao hilo inayotolewa na Serikali.


Kwa upande wake kiongozi wa timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo Bi. Happy Kapinga amesema kuwa hatua  ya timu yake kufika mkoani Lindi kwa ajili ya kutoa elimu hiyo inalenga kuwafanya wakulima hao kuongeza tija kutokana na mkopo huo na hivyo kuongeza kipato chao na mchango wa pato la Taifa kwa ujumla.


"Mkopo huu unaotolewa na Serikali ya awamu ya 6 unajumuisha vifaa vyenye thamani ya shilingi Mil. 1.4 kwa kila mkulima ikiwa ni pamoja na kamba zenye urefu wa mita 70 na upana wa milimita 4, taitai 300, viroba 3 na vigingi 400 ambayo vitamsaidia sana kwenye uzalishaji wa zao la Mwani" Amesema Bi. Kapinga.


Bi. Kapinga amesisitiza kuwa mkopo huo ni wa kipindi cha miaka 5 hivyo kila mkulima anapaswa kurejesha ndani ya muda huo.


Utaratibu huu wa utoaji wa elimu kuhusu mikopo mbalimbali inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi umekuwa ukifanyika mara kwa mara huku ukilenga kuwafanya walengwa kunufaika na mikopo hiyo.

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Happy Kapinga (kushoto) akimfafanulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omari kuhusu mkopo usiona riba wa pembejeo za zao la Mwani unaotolewa kwa wakulima wa mkoa huo muda mfupi baada ya kufika ofisini kwake Juni 07, 2023

Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Happy Kapinga akiwaonesha wakulima wa Mwani kutoka vijiji vya Nachunyu, Mmumbu, Shuka na Sudi mwongozo wa kilimo cha zao hilo wakati wa mkutano uliohusisha elimu ya mkopo usio na riba  wa pembejeo za zao la Mwani uliofanyika kijiji cha Nachunyu mkoani Lindi Juni 07, 2023.

Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Lindi Bw. Jumbe Kawambwa akiwaelimisha wakulima wa zao la mwani kutoka Vijiji vya Nachunyu, Mmumbu, Sudi na Shuka vilivyopo wilaya ya Mtama mkoani Lindi kuhusu mkopo usio na riba wa pembejeo za zao hilo unaotolewa na Serikali kwenye mkutano uliofanyika kijiji cha Nachunyu Juni 07, 2023.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni