Nav bar

Alhamisi, 13 Aprili 2023

SASA NAONA MAONO YA DKT. SAMIA KUPITIA SEKTA YA MIFUGO YANATIMIA-DKT. MPANGO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kasi kubwa aliyoiona kwa upande wa sekta ya Mifugo.


Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo Aprili 12, 2023 mara baada ya kufika kwenye eneo la Shamba la Mifugo la Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza alikotembelea na kukagua Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo unaotekelezwa katika vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) vilivyopo shambani hapo.


"Mhe. Rais alikuwa analalamika sana kuhusu utendaji wa sekta ya Mifugo lakini kwa hili nililoliona leo nakiri wazi kuwa sasa yale maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yanatimia na sasa nipo tayari kwenda kupiga magoti kwake ili bajeti tuongeze vituo vingine na bajeti ya Wizara iongezeke"  Mhe. Dkt. Mpango.


Dkt. Mpango ameongeza kuwa hatua hiyo ya Wizara inatibu changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wanaokadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 hadi 70 ya idadi ya watu wote nchini.


"Kama ni mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya Mifugo sasa ndo yanaanzia hapa kwa sababu haiwezekani sisi kama Taifa tunalojivunia kuwa la 3 kwa mifugo mingi lakini bado uuzaji wa nyama bora nje ya nchi upo chini na nimefurahi mmeamua kuanza kunenepesha ng'ombe wetu wa hapa hapa kwanza" Ameongeza Mhe. Dkt. Mpango.


Kwa Upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemueleza Mhe. Dkt. Mpango kuwa takribani vijana 1600 wanahitimu ngazi mbalimbali za elimu kwa upande wa sekta ya Mifugo na kati yao 150 pekee ndo huingia kwenye mfumo rasmi wa ajira hivyo  lengo la ubunifu huo ni kuwawezesha vijana wanaobaki kujiajiri kupitia shughuli hiyo ya unenepeshaji na uuzaji wa  mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.


"Mhe. Makamu wa Rais kinachofanyika hapa ni matokeo ya juhudi zenu wewe na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa kazi ya kutafuta suluhu ya changamoto ya ajira kwa vijana na kutuwezesha pesa za kutekeleza mpango huu ambao kwa awamu hii umejumuisha vijana 240 kutoka pande mbalimbali za nchi yetu" Amesisitiza Mhe. Ulega.


Naye mmoja wa vijana hao Bi. Loyce Nyamoya mbali na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha kupata fursa hiyo aliwataka vijana wanawake kujitokeza kwa wingi kwenye awamu nyingine ili kuongeza idadi ya wawekezaji wanawake kwenye sekta ya Mifugo.


Mbali na vituo hivyo vilivyopo kwenye shamba la Mabuki, mpango huo pia unatekekelezwa Mkoani Tanga kwenye mashamba ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Buhuri na Mkoani Kagera kwenye Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Kikurula.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) akimpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mara baada ya kuridhishwa na maendeleo ya Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo unaotekelezwa katika Shamba la Mifugo la Mabuki mkoani Mwanza Aprili 11,2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) muda mfupi  baada ya kufika kwenye shamba la Mifugo la Mabuki  panapotekelezwa Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo Aprili 11, 2023.

Meneja wa Shamba la Mifugo la Mabuki Bi. Lini Mwalla (kushoto) akimueleza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) aina ya mifugo iliyopo shambani kwake wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. Mpango shambani hapo Aprili 11,2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tatu kutoka kulia) akitembea kwenye shamba la mifugo la Mabuki  panapotekelezwa Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo muda mfupi baada ya kufika katika Shamba hilo  Aprili 11, 2023. Wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akimueleza jambo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) wakati wa ziara ya Makamu wa Rais aliyoifanya  kwenye shamba la Mifugo la Mabuki  panapotekelezwa Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo lililopo Mkoani Mwanza Aprili 11, 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia) akimuonesha jambo Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene (kushoto) muda mfupi  baada ya Mhe. Dkt. Mpango  kufika kwenye shamba la Mifugo la Mabuki panapotekelezwa Mpango wa Mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana kupitia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo Aprili 11, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni