Nav bar

Jumamosi, 1 Aprili 2023

HALMASHAURI KUANZA KUSIMAMIA UJENZI WA MIRADI YA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ameagiza miradi yote inayotekelezwa na Wizara kwenye Halmashauri zote nchini isimamiwe na Halmashauri husika badala ya Wizara hiyo kama ilivyokuwa hapo awali.


Mhe. Silinde ameyasema hayo wakati akihitimisha ziara yake ya kukagua miradi na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara hiyo aliyoifanya kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo amesema kuwa hatua hiyo imetokana na kuchelewa kukamilika kwa miradi hiyo huku mingine ikiwa katika hatua za awali kabisa.


“Halmashauri zimeshatekeleza miradi mingi sana kwa mafanikio na imekamilika kwa wakati, Afisa kutoka Wizarani hawezi kusafiri umbali mrefu kwenda kusimamia mradi na badala yake anapaswa kufanya ufuatiliaji tu” Amesisitiza Mhe. Silinde.


Mhe. Silinde ameongeza kuwa dhamira yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ni kuhakikisha Miradi yote ya Wizara inakamilika kwa ubora na wakati ili iweze kuwasaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Ziara ya Mhe. Silinde ilianzia katika mkoa wa Lindi ambapo pamoja na mambo mengine alipata fursa ya kufunga mafunzo ya wafugaji jongoo bahari 68 waliopo mkoani humo na ameihitimisha kwa kutembelea kituo cha Ukuzaji Viumbe maji cha Ruhila kilichopo Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

Afisa Uvuvi kutoka Kituo cha ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila kilichopo mkoani Ruvuma Bw. Emmanuel Maneno (aliyeshika beseni) akimuelezea Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto kwake) kuhusu utunzaji wa samaki wazazi muda mfupi baada ya Mhe. Silinde kuwasili kituoni hapo Machi 31,2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akipokea maelezo kuhusu aina ya ng'ombe waliopo kwenye shamba la Mifugo la Nangaramo kutoka kwa Afisa Mifugo wa shamba hilo Bw. Imani Mgalla muda mfupi baada ya kuwasili shambani hapo leo Machi 31, 2023.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akiwalisha samaki chakula kwenye kituo cha Ukuzaji viumbe maji cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kufika kituoni hapo leo Machi 31,2023.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni