Nav bar

Jumamosi, 1 Aprili 2023

​ULEGA ATANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO, UVUVI NCHINI ITALIA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na wadau wa maendeleo kutoka taasisi na makampuni mbalimbali nchini Italia na kujadiliana nao fursa mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kuwekeza nchini Tanzania hususan katika sekta ya mifugo na uvuvi.


Waziri Ulega amekutana na wadau hao  jijini Rome wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Italia iliyoanza Machi 30, 2023.


Wakati akiongea kwa nyakati tofauti na washirika hao wa maendeleo, Mhe. Ulega aliwaeleza kuwa, kwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka katika kufanya shughuli zao kiasili na kujiendesha kibiashara ili kuongeza uzalishaji wake.


Aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha sekta hizo mbili zinabadili mfumo wake wa utekelezaji kuwa wa kibiashara, Serikali inatekeleza Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2022/2023-2026/2027 na Mpango Kambambe wa Maendeleo wa Sekta ya Uvuvi wa Mwaka 2021/2022-2036/2037.


“Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan  amedhamiria kubadilisha mfumo wa uzalishaji wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka katika kufanya shughuli zake kiasili na kujiendesha kibiashara ili kuongeza uzalishaji wake, hivyo, kukutana kwetu leo ni fursa nzuri ya kujadiliana nanyi ili muweze kuona fursa za uwekezaji  katika sekta hizo mbili ambazo kufanikiwa kwake kunahitaji ushiriki wenu”, alisema Ulega


Halikadhalika, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo pia kuwaeleza wadau hao kuwa serikali ya Tanzania ingependa kupata wawekezaji mahiri katika sekta ya mifugo hususan eneo la biashara ya nyama kwa kushirikiana na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani katika sekta za mifugo na uvuvi hususan zao la dagaa kutoka ziwa Victoria.


Kwa upande wa Mkurugenzi wa Italia, anayeshughulikia nchi za Afrika, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta alikubali ombi la Waziri Ulega la kuiweka nchi ya Tanzania miongoni mwa nchi za kipaumbele katika masuala ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Aidha, Waziri Ulega alisema kuwa anatambua ushirikiano uliopo baina ya serikali na wawekezaji kutoka nchini Italia katika kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania huku akiwakaribisha wawekezaji wengi zaidi kufanya uwekezaji nchini humo.


Katika ziara yake hiyo, Waziri Ulega alikutana na viongozi wa taasisi ya SACE, Benki ya Uwekezaji ya Italia (CDP), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), COGEMAT Slaughtering and Meat Technology na Mkurugenzi wa Italia, anayeshughulikia nchi za Afrika, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), (wa nne kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Nchi za Afrika - Italia, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta (wa tano kutoka kushoto) na Balozi wa Tanzania Nchini Italia  Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (wa pili kutoka kushoto) mara baada ya kikao chao kilichofanyika Ofisini kwa Balozi Giuseppe nchini Italia Machi 30, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), (katikati kushoto) akizungumza na Wataalam wa Benki ya Uwekezaji ya Italia (CDP - Italian Development Finance Institution) wakiongozwa na ndugu Giulio Dal Magro, Mkuu wa Fedha za Maendeleo CDP (wa tatu kutokea kulia) wakati wa kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za CDP Jijini Roma, nchini Italia Machi 30, 2023. Pamoja na mambo mengine Mhe. Ulega aliwaeleza kuhusu fursa kubwa ya kushirikiana na Wawekezaji iliyopo nchini Tanzania kwenye mnyororo wa thamani katika Sekta za Mifugo na Uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), (kulia) akiwa katika picha pamoja na  Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia Machi 30, 2023.


Waziri wa Mifugo Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), (kulia)  akizungumza na Mkurugenzi wa Italia anayeshughulikia Nchi za Afrika, Mhe. Balozi Giuseppe Mistretta,  wakati wa kikao walichokifanya kwenye Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zilizopo jijini Rome, Italia Machi 30, 2023. Kikao hicho kililenga kujenga uhusiano kati ya Tanzania na Italia na kuangazia fursa za uwekezaji kwa Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Waziri alimuomba Mhe. Giuseppe kuwa Tanzania iwemo katika nchi za Kipaumbele kwa Italia katika masuala ya miradi mbalimbali ya Maendeleo na Mhe. Balozi Giuseppe amekubali kufanya hivyo .

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), (wa pili kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa COGEMAT, Ndugu Arena, (wa kwanza kulia) na Kiongozi wa Bergs and More, Bi. Rita Ricciardi mara baada ya kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia Machi 30, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni