Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemuhakikishia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kuwa Sekta za Mifugo na Uvuvi zinakwenda kuongeza uzalishaji, kutoa ajira na kuleta tija kwa taifa.
Waziri Ulega ameyasema
hayo leo (28.02.2023) mara baada ya kukabidhiwa ofisi na Waziri aliyemaliza
muda wake Mhe. Mashimba Ndaki kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Mji wa
Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Amesema kuwa zipo
fursa nyingi kupitia Sekta za Mifugo na Uvuvi ambazo zikitumiwa vizuri na
vijana zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kutoa ajira na kuongeza mchango
wa sekta hizo kwenye pato la taifa. Hivyo amewasihi watumishi kufanya kazi kwa
uweledi, ubunifu, uaminifu na kuongeza kasi katika utendaji.
Aidha, amewashukuru
viongozi waliomaliza muda wao kwa ushirikiano ambao walimpatia wakati wote
aliohudumu kama Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambapo pia amewasihi watumishi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi ili mikakati iliyowekwa ya kuendeleza
sekta hizo.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Mhe. David Silinde ameishukuru Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) kwa ushirikiano waliompatia wakati akitekeleza majukumu
yake lakini amewasihi watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na
viongozi wote wapya ili kuhakikisha maendeleo kwenye sekta yanakua.
Mhe. Silinde amesema wameletwa
kwenye Wizara kwa ajili ya kuhakikisha inatangazwa kutokana na kazi mbalimbali
zinazofanywa ili wadau waweze kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta za Mifugo na
Uvuvi.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewasihi watumishi kutoa ushirikiano
katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Amewasihi watumishi kutoa ushauri
utakao saidia kuzifanya sekta za mifugo na uvuvi zinaendelea kukua na kuzalisha
kwa tija. Pia amewasihi watumishi watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu
na upendo.
Naibu Katibu Mkuu
anayesimamia Sekta ya Mifugo, Dkt. Daniel Mushi amesema kuwa kazi waliyonayo ni
kuhakikisha wanaendelea kusimamia utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta
ili kuhakikisha uzalishaji wa mifugo na mazao yake unaleta tija kwa wafugaji na
taifa kwa ujumla. Pia amesema kuwa Wizara itaendelea na jitihada ya kuimarisha
taasisi zilizo chini yake ili kuhakikisha zinaendelea kutimiza wajibu wake
katika kuleta maendeleo yanayotarajiwa.
Naibu Katibu Mkuu
anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Bi. Agness Meena amesema kuwa matarajio yake ni
kuhakikisha kwanza wanasimamia utekelezaji wa mikakati ambayo tayari
imeshawekwa na viongozi waliotangulia katika kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inakua.
Waziri aliyemaliza
muda wake, Mhe. Mashimba Ndaki amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kumpatia
nafasi ya kusimamia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Vilevile amewashukuru watumishi
wote kwa ushirikiano waliompatia wakati wa utekelezaji wa majukumu n ani Imani
yake kuwa ushirikiano huo utaendelea kutolewa kwa viongozi wapya.
Mhe. Ndaki amewasihi
viongozi kushirikiana na watumishi katika kutekeleza majukumu yao ili sekta za
mifugo na uvuvi ziweze kukua na kuongeza mchango wake kwa wafugaji, wavuvi na
pato la taifa kwa ujumla. Vilevile amewaeleza kuwa Mhe. Dkt. Samia ameendelea kusisitiza
kuwa Sekta za uzalishaji ikiwemo Mifugo na Uvuvi zihakikishe zinazalisha ajira
kwa vijana na wanawake hivyo bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanyika.
Naye Katibu Mkuu
Mstaafu aliyekuwa anasimamia Sekta ya Mifugo amewashukuru viongozi na watumishi
kwa ushirikiano waliompatia katika utekelezaji wa majukumu. Pia amewasihi
watumishi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya walioteuliwa ili
kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kukua.
Dkt. Rashid Tamatamah
ambaye alikuwa Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi licha ya kuwashukuru
watumishi kwa ushirikiano waliompatia amewaasa viongozi kuendelea kusimamia
maslai ya watumishi ili waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya watumishi, Afisa Uvuvi Mkuu, Bi. Upendo Hamidu
amewashukuru viongozi waliomaliza muda wao kwa ushirikiano walioutoa katika
kutekeleza majukumu ya Wizara na ameahidi kuwa watumishi wataendelea kutekeleza
majukumu yao ili kuhakikisha Sekta za Mifugo na Uvuvi zinakuwa ni kimbilio
kwenye kutoa ajira kwa vijana na wanawake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni