Nav bar

Jumatano, 7 Desemba 2022

 WADAU WAHIMIZWA KUUNGA MKONO MPANGO WA MABADILIKO SEKTA YA MIFUGO 


Na Mbaraka Kambona, Iringa


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wadau wa sekta ya mifugo wakiwemo wafugaji kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo ili kufanikisha nia ya Serikali ya kuwezesha wananchi kufuga kisasa.


Mhe. Ndaki alitoa rai hiyo wakati akizindua mradi wa ufugaji bora unaofadhiliwa na Shirika la World Vision katika Kata ya Maduma na Nyololo zilizopo Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa Disemba 5, 2022.


Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo ambao lengo lake ni kuwawezesha wadau wa sekta hiyo kufuga kwa tija zaidi ya ilivyo sasa.


"Mhe. Rais, Dkt. Samia anataka kuona ufugaji wetu tunaofanya unakuwa wa kibiashara na unaleta  tija kubwa kwa wafugaji", alisema Mhe. Ndaki


Aliongeza kwa kusema kuwa mradi wa ufugaji bora  wananchi unaotekelezwa na Shirika la World Vision unaunga mkono mpango wa mabadiliko wa sekta ya mifugo hapa nchi huku akiwahimiza wadau wengine kujitokeza kushirikiana na Serikali katika kufanikisha lengo hilo.


Alisisitiza kuwa kupitia mpango huo wanakwenda kuboresha ufugaji nchi nzima huku akiongeza kuwa mwaka ujao wa fedha wataendelea kugawa mitamba katika Wilaya nyingine zaidi.


Aidha, Waziri Ndaki alisema kuwa ili mpango huo uweze kufanikiwa vizuri ni wajibu wa kila mfugaji kuwa na fikra za ufugaji bora unaoendana na mabadiliko ya tabia nchi.


"Ardhi yetu tuliyonayo sasa hairuhusu tena kufanya ufugaji wa kuhamahama, hivyo ni vyema tukawa na fikra za kubadili mtindo wa ufugaji wetu," alifafanua 


Kwenye hafla hiyo,  Mhe. Ndaki aligawa mitamba 300 kwa wafugaji ili waanze kufuga kisasa kwa lengo la kujipatia lishe blora na kukuza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiagwa kwa furaha  na sehemu ya wanufaika wa Mradi wa Ugawaji wa mitamba muda mfupi baada ya kugawa mitamba 300 kwa wanufaika hao katika hafla fupi iliyofanyika Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa Disemba 5, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na wananchi wa Kata ya Nyololo na Maduma, Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa alipofanya ziara ya kikazi Disemba 5, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiongozana na Mbunge wa Mufindi Kusini, Mhe. David Kihenzile (wa pili kutoka kulia) alipokuwa akienda kumtembelea mmoja wa wanufaika wa Mradi wa Ugawaji mitamba unaofadhiliwa na Shirika la World Vision Tanzania katika Kata ya Nyololo na Maduma Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa Disemba 5, 2022.Wengine katika picha ni baadhi ya Viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mufindi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akimkabidhi Mtamba mmoja wa Wananchi walionufaika na mradi wa Ugawaji wa mitamba kwa wananchi wa Kata ya Nyololo na Maduma, Wilayani Mufindi, Mkoani Iringa ili wafanye ufugaji wa kisasa na kujikwamua kiuchumi. Mradi wa ufugaji bora unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la World Vision Tanzania. Mhe. Ndaki alikabidhi Mitamba hiyo 300 Disemba 5, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi muda mfupi baada ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. Saad Mtambule. Mhe. Ndaki alikuwa na ziara ya siku moja katika Wilaya hiyo aliyoifanya Disemba 5, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi muda mfupi baada ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. Saad Mtambule. Mhe. Ndaki alikuwa na ziara ya siku moja katika Wilaya hiyo aliyoifanya Disemba 5, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni