Nav bar

Jumatano, 7 Desemba 2022

ULEGA: WIZARA IMEJIPANGA KUBORESHA LISHE YA WANANCHI

Na Mbaraka Kambona, 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake inalo jukumu la kuhakikisha mazao yanayozalishwa katika sekta za mifugo na uvuvi yanaendelea kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uhakika wa chakula, kuboresha hali ya lishe ya wananchi na kuinua kipato cha wananchi na nchi kwa ujumla.


Mhe. Ulega aliyasema hayo katika Mkutano wa Nane wa Wadau wa Lishe Tanzania uliofanyika Mkoani Mara Disemba 6, 2022.


Alisema ni wazi kuwa, mazao ya mifugo na uvuvi ni chanzo muhimu cha protini yenye thamani ya juu kibaolojia, vitamini mbalimbali kama vile A, B na D, madini muhimu kama vile madini ya chuma, madini ya calcium na madini ya zinki, yote haya ni muhimu kwa lishe na afya bora ya mwanadamu. 


“Sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tunalo jukumu la kuhakikisha  mazao yatokanayo na mifugo na uvuvi yanaendelea kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uhakika wa chakula nchini, yanaboresha hali ya lishe ya wananchi na kuinua kipato cha wananchi na nchi kwa ujumla,”alisema


Alibainisha kuwa wizara imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali zinazochangia kuboresha hali ya lishe nchini ikiwemo kuhamasisha ulaji na utumiaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kupitia majukwaa mbalimbali kwa kushirikiana na wadau pamoja na sekta binafsi.


Aidha, Waziri Ulega alisema kuwa wizara imeendelea kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo nchini kupitia ununuzi na usambaji wa madume bora ya mbegu kwa wananchi, uhimilishaji, uzalishaji na usambaji wa mitamba ya ng’ombe bora wa maziwa na uanzishaji wa vituo atamizi vya ufugaji kwa vijana. 


“Katika kuhakikisha mazao haya yanawafikia wananchi wizara imeendelea kujenga vituo vya kukusanyia maziwa, ujenzi wa vituo vya unywaji maziwa shuleni, na uhamasishaji wa uzalishaji wa wanyama wadogo katika kaya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na Halmashauri,”alifafanua 


Halikadhalika, Mhe. Ulega alibainisha kuwa wizara imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mazao ya uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi na wakuzaji viumbe maji zana na pembejeo zikiwemo boti, vizimba vya kufugia samaki, vifaranga na chakula cha samaki kwa ajili ya kuongeza uzalishaji. 


Waziri Ulega alisema kuwa wizara imeainisha mchango wake katika kuimarisha lishe kupitia viashiria saba (7) vilivyowekwa katika Mpango wa Pili Jumuishi wa Lishe Kitaifa unaotekelezwa katika kipindi cha miaka 5 (2021/22-2025/26) huku akiwahimiza wadau mbalimbali wakiwemo, wadau wa maendeleo, wafugaji, wavuvi, wasindikaji na wafanyabiashara wa mifugo, uvuvi na mazao yake kushirikiana na Wizara katika kuhakikisha kuwa sekta za Mifugo na Uvuvi zinachangia katika kuimarisha hali ya lishe nchini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalim, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima(katikati) akiwa ameshika Kitabu cha Mpango wa Lishe (2022/2027) muda mfupi baada ya kuuzindua mpango huo katika Mkutano wa Nane wa Wadau wa Lishe uliofanyika Mkoani Mara Disemba 6, 2022. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. Wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde. Dkt. Gwajima alimuwakilisha Waziri Mkuu katika mkutano huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akitoa salamu za Wizara  katika Mkutano wa Nane wa Wadau wa Lishe uliofanyika Mkoani Mara Disemba 6, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni