Nav bar

Jumatano, 7 Desemba 2022

ULEGA AHIMIZA WATANZANIA KUTUMIA BIDHAA ZA NDANI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Mhe. Ulega ameyasema hayo leo (03.12.2022) muda mfupi baada ya kuteuliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) kuwa balozi wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini tukio lililofanyika kwenye Ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar-es-salaam.


“Hatuzuii wazalishaji  wengine kuingiza bidhaa zao hapa nchini kwa sababu hata siku moja hatujawahi kuogopa ushindani na tunaamini kupitia ushindani ndio tunapata fursa ya kuendelea kutengeneza bidhaa zenye ubora zaidi” Ameongeza Mhe. Ulega.


Mhe. Ulega amesema kuwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa hivi sasa zina viwango vinavyoweza kushindana na bidhaa yoyote inayotoka nje yanchi ambapo aliwapongeza wazalishaji hao ikiwa ni pamoja na wasindikaji wa bidhaa za maziwa kwa kutengeneza maziwa yanayoweza kukaa muda mrefu bila kuharibika.


“Na sio hilo tu, hivi sasa kampuni ya Maziwa ya Asas ipo mbioni kutengeneza maziwa ya unga hatua ambayo itatufanya kama nchi kupiga hatua kubwa sana kwa upande wa teknolojia ya maziwa na haya yote yanatokana na jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wetu wa ndani na nje” Amesema Ulega.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) Bi. Latifa Khamis amesema Mamlaka yake imeamua kumteua Mhe. Ulega kuwa balozi  wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kutokana na jitihada kubwa za kizalendo zinazofanywa na Mhe. Ulega kwa kutangaza miradi mbalimbali ya Maendeleo inayofanyika hapa nchini.


“Maonesho haya ya Bidhaa zinazozalishwa nchini yanaanza leo na yatarajiwa kukamilika baada ya Wiki moja na lengo kuu ni kuwahamasisha watanzania kutumia zaidi bidhaa zinazotengenezwa na wawekezaji waliopo hapa nchini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.


Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya amesema kuwa tasnia ya maziwa ni moja ya maeneo makubwa nchini yanayozalisha ajira kwa wingi hivyo amewataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye tasnia hiyo.


“Lakini pia nitoe angalizo wakati tukitumia fursa hizo tunapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na Bodi ya Maziwa na miongoni mwao msitumie chupa za plastiki zilizotumika kuhifadhia maji au vimiminika vingine  kwa ajili ya kuhifadhia maziwa kwa sababu ni kinyume na taratibu za ufungashaji wa maziwa na ni hatari kwa afya ya mtumiaji” Amehitimisha Dkt. Msalya.


Ufunguzi wa Maonesho hayo ulitanguliwa na mbio za hiyari zilizoongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega na   Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) Bi. Latifa Khamis ambapo zaidi ya vikundi 8 vya wakimbiaji vilishiriki.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) Bi. Latifa Khamis (kulia) na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya (kushoto) wakifanya mazoezi ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofanyika wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Bidhaa zinazozalishwa nchini uliofanyika leo (03.12.2022) jijini Dar-es-Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) Bi. Latifa Khamis (kushoto) akimkabidhi cheti Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mara baada ya Mhe. Ulega kushika nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya mbio fupi yaliyofanyika kama ishara ya ufunguzi wa Maonesho ya Bidhaa zinazozalishwa nchini uliofanyika leo (03.12.2022) jijini Dar-es-Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade) Bi. Latifa Khamis (kulia) na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya (kushoto) wakishiriki mbio fupi  ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofanyika wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Bidhaa zinazozalishwa nchini uliofanyika leo (03.12.2022) jijini Dar-es-Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni