◼️ Nigeria yaeleza ilivyofanikiwa kukomesha soko la ngozi yake..
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita yatakayolenga uzalishaji na ustawi wa wanyama aina ya Punda ambao wameonekana kuwa kwenye hatari ya kutoweka.
Katika hotuba yake iliyosomwa leo (02.12.2022) kwa niaba yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba wakati wa kufunga Mkutano wa zaidi ya nchi 20 wanachama wa Umoja wa Afrika, Mhe. Majaliwa amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali ili kulinda ustawi wa wanyama hao, idadi yao imeendelea kupungua na mkazo kutoka kwa jamii na wadau wengine ni kidogo.
“Hivyo ninaagiza kuwe na juhudi za dhati kuwekeza kwenye uzalishaji wa punda kupitia mashamba makubwa, madogo na ya kati ikiwa ni pamoja na Wizara kutengeneza mpango mkakati wa kuzalisha na kuendeleza Punda hapa nchini” Ameongeza Mhe. Majaliwa.
Agizo jingine lililotolewa na Mhe. Majaliwa ni kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau mbalimbali kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji wa punda ili watu wengine wenye nia ya kufuga wanyama hao kwa ajili ya kufanya biashara na shughuli za kijamii waweze kufanya hivyo.
“Lakini pia niagize Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini ifanye utafiti juu ya chagamoto zinazoikabili tasnia ya ufugaji wa punda na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo na pia itolewe elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa punda, matunzo na fursa zilizopo katika ufugaji wa wanyama hao” Amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Akizungumzia namna Wizara yake itakavyotekeleza maagizo hayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa tayari Wizara yake imeanza kutekekeza maelekezo yote ikiwa ni pamoja na kwa kuwajumuisha punda kupitia sheria ya utambuzi wa wanyama ambayo itaipa Wizara hiyo fursa ya kufahamu idadi ya punda waliopo hapa nchini kwa kadri watakavyokuwa wanaongezeka.
“Lakini pia mkutano wetu huu umetoka na mapendekezo ambayo kwa kushirikiana na wataalam wa nchi zote za Afrika yanapaswa kuwekwa vizuri na kupelekwa kwenye nchi zote zilizoshiriki katika mkutano huu na hata zile ambazo hazikushiriki kisha tuone namna yanavyoweza kutekelezwa na kila nchi” Ameongeza Mhe. Ndaki.
Mhe. Ndaki ametaja baadhi ya mapendekezo hayo kuwa ni pamoja na nchi zote za Afrika kutengeneza mfumo wa ulinzi wa wanyama hao ikiwa ni pamoja na kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza azimio hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kutoka nchini Nigeria Dkt. Maimuna Abdullah mbali na kupongeza hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kudhibiti utowekaji wa Punda amesema kuwa biashara ya ngozi ya punda imeshuka kutoka Naira 300,000 ya awali hadi Naira elfu 40 mwezi huu baada ya Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Vipodozi nchini humo kupiga marufuku bidhaa zote zinazotokana na ngozi ya punda.
Mkutano huouliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda barani Afrika umehitimishwa leo ambapo viongozi na watendaji kutoka zaidi ya nchi 20 wanachama wa Umoja wa Afrika wamefikia maadhimio kadhaa yanayolenga kuongeza idadi na ustawi wa wanyama hao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akisoma hotuba ya kufunga Mkutano wa zaidi ya mataifa 20 wanachama wa Umoja wa Afrika (hawapo pichani) uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda jijini Dar-es-Salaam leo (02.12.2022).
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga (kushoto) akielezea namna Tanzania inavyotekeleza maazimio ya kudhibiti utowekaji wa wanyama aina ya Punda muda mfupi kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa zaidi ya nchi 20 wanachama wa Umoja wa Afrika uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama hao leo (02.12.2022) jijini Dar-es-Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni