Wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 4.4 kwa ajili ya kuanzishwa kwa vituo atamizi kusaidia vijana kwenye Ufugaji wenye tija.
Wanamichezo hao wametoa pongezi hizo Oktoba 13,2022 walipotembelea Kituo atamizi kimojawapo kilichopo Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kituo cha Tanga (Buhuri) kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho ikiwemo mpango huo unaotambulika kwa jina la Samia Ufugaji Kwa Tija (SAUTI).
Akitoa ufafanuzi wa kuhusu utekelezaji wa mpango huo ambao tayari umeshaanza na vijana 60 ambao wanaendelea kupata mafunzo katika kituo hicho Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa Mradi huo una lengo la kuwainua vijana kupitia ufugaji wenye tija ambapo vijana hao watapatiwa mitaji watakapomaliza mafunzo.
"Tuna jumla ya vituo atamizi 8 ambapo vitatu vipo Tanga na Kati ya hivyo viwili vipo LITA Buhuri na kimoja kipo TALIRI Tanga, kwa sasa vijana wenyewe wanajenga Banda la kunenepeshea mifugo wakikamilisha wanakwenda kutafuta Ng'ombe wao wenyewe minadani kwa Wafugaji huko na kuanza kufuga, hapa watasaidiwa kupatiwa Ng'ombe hao lakini pia tutawanunulia matrekta watalima wenyewe, watapanda na kuvuna majani na visima tutawachimbia wamwagilie majani." Amesema Dkt. Mwambene.
Akizungumzia kuhusu mgawanyo wa Ng'ombe kwa vijana hao, Dkt. Mwambene amesema kuwa kila kijana kwa mwaka atakuwa amewezeshwa kufuga jumla ya Ng'ombe 40.
"Kila kituo kitakuwa na Ng'ombe 300 kwa wakati mmoja na katika Ng'ombe hao kila kijana atapewa Ng'ombe 10 ndani ya miezi mitatu, kwaiyo kwa mwaka mzima akibahatika atakuwa amefuga mara nne hivyo atakuwa amefuga Ng'ombe 40." Ameongezea Dkt. Mwambene.
Akizungumza kwa niaba ya Wanamichezo hao, Mwenyekiti wa Michezo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Ndugu Ally Suru amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya Mradi huo utakaowasaidia vijana kujiajiri.
"Namba ya vijana wanaohitimu masomo vyuoni ni kubwa sana Serikali na Sekta binafsi haiwezi kuwaajiri wote moja kwa moja, kwaiyo silaha kubwa ya vijana wetu kupata ajira ni kujiajiri wenyewe, hivyo wazo hili la Rais Samia la Ufugaji kwa tija ni la msingi sana kwa vijana hawa na sasa nitakuwa balozi mzuri kulisemea hili." Amesema Suru.
Akizungumza kwa niaba ya Vijana hao ambao ni wahitimu wa fani mbalimbali za Mifugo kutoka LITA na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Bw. Castor Edson Mwakasumba amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwachagua kuwa miongoni mwa wanufaika wa Mradi huo.
"Tunamshukuru Rais Samia kwanza kwa kutuchagua kuwa miongoni mwa wanufaika wa Mradi huu kwa sababu tumesikia tuliomba wengi, lakini pia kutupatia hizi fedha tunaahidi kushiriki na kufanikisha kwa asilimia mia moja, pia tunawashukuru kwa kuja kututia moyo." Amesema Mwakasumba.
Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia LITA na TALIRI imepanga kuanzisha na kuendesha mafunzo ya mifugo kibiashara kupitia vituo atamizi nane. Vituo hivyo vinaanzishwa katika mikoa mitatu ya Tanga, Mwanza na Kagera ambapo washiriki wenye sifa 240 watanufaika na mpango huu. Lengo la mpango huu ni kutoa mafunzo ya ufugaji kibiashara kwa vitendo ili kuwajengea uwezo, ujuzi na ujasiri wa kuanzisha miradi ya ufugaji yenye tija na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na mchango wa sekta kwenye pato la Taifa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Dkt. Pius Mwambene na wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Vijana wanaoendelea na Mafunzo kupitia mpango wa Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI) Oktoba 13,2022 walipofika kutembelea Kituo cha LITA (Tanga) kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Dkt. Pius Mwambene (kulia) akikabidhi vinjwaji kwa Mwenyekiti wa Michezo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Ndugu Ally Suru kwa niaba ya wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) Oktoba 13,2022 walipofika kutembelea Kituo cha LITA (Tanga) kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Dkt. Pius Mwambene (kushoto) akizungumza na wanamichezo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Oktoba 13,2022 walipowasili Kituo cha LITA (Tanga) kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wakala hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni