Nav bar

Jumatano, 19 Oktoba 2022

NZUNDA: UDHIBITI WA MAGONJWA KWA MIFUGO NI LAZIMA

Na Mbaraka Kambona,


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa suala la udhibiti wa magonjwa kwa mifugo sio la hiyari, ni la lazima, hivyo kila mfugaji ahakikishe anachanja na kuogesha mifugo yake kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam ili kuiepusha mifugo na magonjwa.


Nzunda alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha program ya mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo jijini Dar es Salaam  Oktoba 13, 2022. 


"Suala la udhibiti wa magonjwa ya mifugo kwa mfugaji sio la hiyari, ni jambo la lazima,  chanjo kwa mifugo sio jambo la hiyari, kuogesha sio jambo la hiyari, ukiwa mfugaji ni lazima kuhakikisha unafuata ratiba ya kitaalam ya uogeshaji ili kudhibiti magonjwa",alisema


Aliwataka Wakurugenzi wanaosimamia huduma za mifugo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha wanasimamia maelekezo hayo na kuzingatia Sheria zilizopo ili mifugo ihudumiwe inavyopaswa.


"Mfugaji ambaye atakiuka,  hatua za kisheria na za kiutawala zichukuliwe, na pale ambapo kuna kutokuelewa, elimu ya kina itolewe ili wananchi na viongozi waelewe umuhimu wa kudhibiti magonjwa kwa mifugo",  aliongeza


Aidha, aliwataka madaktari hao waliohitimu mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo kuhakikisha wanaenda kutumia ujuzi, maarifa na uzoefu walioupata katika kuchukua hatua za kudhibiti magonjwa nchini.


Kikao cha program ya mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo kilifanyika jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kuanzia Oktoba 11 hadi 13, 2022, na  Washiriki wa program hiyo  ni maafisa mifugo kutoka ngazi ya Wizara, Halmashauri na Taasisi za Mafunzo.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa kikao cha program ya mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo muda mfupi baada ya kufunga rasmi kikao hicho jijini Dar es Salaam  Oktoba 13, 2022.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda(kushoto) akiongea  na Mwakilishi wa Shirika la misaada la Kimarekani la USAID, Bi. Carrie Read muda mfupi baada ya kufunga kikao cha program ya mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo  jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 13, 2022.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga akitoa maelezo ya utangulizi wakati wa kikao cha program ya mafunzo rejea ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo kilichofanyika  jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 11-13, 2022. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni